Marekani inatarajiwa kujiondoa rasmi hii leo kutoka Shirika la Afya Duniani WHO, hatua ambayo imeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wataalam wa afya na jumuiya ya kimataifa.
Hatua hiyo imekuja licha ya tahadhari kwamba kujiondoa kwa taifa hilo lenye ushawishi mkubwa duniani, kutadhoofisha uwezo wa Marekani kukabiliana na majanga ya kiafya, pamoja na kuathiri juhudi za kimataifa za kudhibiti milipuko ya magonjwa.
Uamuzi huo pia unatajwa kukiuka sheria za ndani za Marekani, ambazo zinaitaka serikali ya Washington kulipa deni la takriban dola milioni 260 kwa WHO kabla ya kujiondoa rasmi.
Kulingana na sheria hiyo, Marekani inapaswa kutoa notisi ya mwaka mmoja na kuhakikisha imekamilisha malipo yote inayodaiwa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa.
Rais Donald Trump alitangaza nia ya kujiondoa kutoka WHO siku ya kwanza ya urais wake mwaka 2025 kupitia amri ya kiutendaji, akilalamikia kile alichokitaja kuwa udhaifu wa shirika hilo katika kushughulikia majanga ya kiafya.
Utawala wa Trump umekuwa ukiishutumu WHO kwa kushindwa kudhibiti na kusambaza taarifa muhimu kwa wakati, jambo ambalo, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, limeigharimu nchi hiyo mamilioni ya dola.



