Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imezitangazia taasisi zote za umma na serikali zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi kujisajili ndani ya miezi mitatu ili kutekeleza wa maagizo ya Serikali yaliyotolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt
Emmanuel Mkilia amesema , taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au/na kuchakata taarifa binafsi ambazo bado
hazijakamilisha usajili wake PDPC imewapatia miezi mitatu ya nyongeza
kuanzia Januari 8 hadi Aprili 8 2026 kuhakikisha zinakamilisha usajili kwa hiari ndani ya kipindi hicho.

‘’Tume inasisitiza kuwa kipindi hiki hakimaanishi kusitishwa kwa utekelezaji wa Sheria, bali ni dirisha la mwisho la muda wa hiari kabla ya hatua kali kuchukuliwa kwa taasisi ambazo zitakuwa hazijakamilisha usajili kwa mujibu wa Sheria’’amesema.

Dkt Mkilia amesema PDPC inapenda kuujulisha umma kuwa, baada ya dirisha la mwisho la muda wa hiari kuisha itaanza mara moja ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria kwa tansisi za umma na binafsi, zinazokusanya
au/na kuchakata taarifa binafsi.

Aidha Ukaguzi huu utahusisha kubaini taasisi za umma na binafsi zinazokukusanya, kuhifadhi, kuchakata, na kusafirisha taarifa binafsi nje ya nchi bila kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 na Kanuni zake.

‘’ PDPC inatoa taarifa kwamba taasisi ikibainika inakwenda kinyume hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote, taasisi au kampuni itakayobainika kukiuka Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 katika utekelezaji wa shughuli zake.

Kwa mujibu wa Sheria tajwa, hatua hizo ni pamoja na kurozwa faini, kifungo, au vyote kwa pamoja, pamoja na kulipa fidia kwa wote
watakaoathirika kutokana na ukiukwaji wa matakwa ya Sheria.

Vilevile, mtu au taasisi yoyote itakayobainika kuvunja faragha au kutumia taarifa binafsi bila ridhaa ya mhusika wa taarifa hizo, au
kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria, atawajibishwa ipasavyo bila kujali hadhi au ukubwa wake’’amesema

PDPC inatoa wito kwa taasisi zote za umma na binafsi kuchukua hatua za haraka kujisajili, kuimarisha mifumo yao ya ulinzi wa taarifa binafsi, na kuhakikisha uzingatiaji kamili wa Sheria ikiwa ni wajibu wao kwa Serikali wa kulinda haki za kikatiba za wananchi, hususan haki ya faragha katika uchumi wa kidijitali.

Aidha, katika kuimarisha uelewa wa umma na wadau kuhusu haki na wajibu unaotokana na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) inapenda itaungana na mataifa mengine duniani
kuadhimisha Wiki ya Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi

Amesema lengo ni kukuza uelewa na mshikamano wa dunia katika kulinda
haki ya faragha,kwa mwaka 2026, maadhimisho haya yatafanyika kuanzia
tarehe 26 hadi 30 Januari, huku kilele chake kikiwa ni tarehe 28

Katika kipindi hicho, PDPC itatekeleza programu maalumu za elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari vya kitaifa na kijamii, kutoa mafunzo kwa taasisi za umma na binafsi, pamoja na kufanya ziara za kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ili kuwafikia wananchi moja kwa moja.

Amesema maadhimisho hayo yataongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki
zao kama wahusika wa taarifa binafsi, kuhimiza uwajibikaji wa taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi, na kujenga utamaduni wa kulinda faragha kama nguzo muhimu ya matumizi salama ya teknolojia na huduma za kidijitali.

Aidha Tume itaendelea kutekeleza jukumu lake kwa uadilifu, weledi na bila upendeleo, kwa lengo la kulinda taarifa binafsi za Watanzania na kujenga mazingira salama ya matumizi ya teknolojia na huduma za
kidijitali.