Umoja wa Afrika umetangaza kuiondolea Guinea vikwazo ilivyoiwekea kufuatia mapinduzi ya mwaka 2021, baada ya nchi hiyo kuandaa uchaguzi wa rais mwezi Desemba.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limesema Guinea imepiga hatua katika utekelezaji wa mkakati wa kipindi cha mpito ambacho kiliishia kwa kuandaliwa kwa uchaguzi wa mwezi uliopita.
Umoja huo wa Afrika umempongeza kiongozi wa zamani wa jeshi Mamady Doumbouya kwa kuchaguliwa kwake. Doumbouya aliapishwa kama rais Jumamosi iliyopita mbele ya maelfu ya wafuasi wake na marais kadhaa.
Doumbouya alimpindua rais Alpha Conde mwaka 2021 na tangu aingie madarakani aibinya uhuru wa kiraia na kupiga marufuku maandamano.
Wapinzani wake wa kisiasa wamekamatwa, kufunguliwa mashtaka au kukimbilia uhamishoni.



