Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yya Mapinduzi Zanzibar zimejipanga kuhakikisha zinanufaika vyema na fursa za programu za miradi na mikataba ya kimataifa kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Rai hiyo imetolewa Januari 22, 2026 Mjini Zanzibar na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi wakati wa ziara yake aliyoifanya kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.
Dkt. Muyungi amesema masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabiachi yamekuwa na fursa kubwa duniani kwa sasa na kwa kutambua umuhimu na uliopo Tanzania imejipanga kikamilifu kuhakikisha fursa hizo zinawanufaisha Watanzania.
Akitolea mfano amesema kwa sasa biashara ya kaboni duniani inazalisha kiasi cha dola trilioni 1.3 pesa na hivyo kuwa ni mojawapo ya biashara muhimu ya kiuchumi kwa mataifa mbalimbali ambayo Tanzania pia imeipa msukumo wa kutosha katika kuinufaisha jamii.

“Biashara ya kaboni kwa sasa ni fursa adhimu kwa sasa duniani, jambo kubwa lenye umuhimu ni kuhakikisha tunawajengea uwezo Wataalamu wetu badala ya kutumia washauri elekezi na hii itasaidia kubaini kiwango halisi cha kaboni na faida za kifedha zinazoweza kupatikana” amesema Dkt. Muyungi.
Amesema katika kuhakikisha biashara ya kaboni italeta manufaa makubwa kwa Watanzania, Serikali tayari imekijengea uwezo Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) sambamba na kujenga uwezo kwa wataalaam waliopo.
“NCMC kwa sasa ipo rasmi na tayari menejimenti yake imekabidhiwa vitendea kazi muhimu ikiwemo magari ili kuanza shughuli zake katika kubaini na kuanisha fursa za biashara ya kaboni na kutoa elimu kwa wananchi” amesema Dkt. Muyungi.
Aidha Dkt. Muyungi amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kufanikisha upatikanaji wa fedha na uandishi wa maandiko ya miradi ya mazingira na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema katika bara la Afrika kwa sasa, Zanzibar imekuwa nchi ya kwanza inayoongoza katika uzalishaji wa zao la mwani ambalo linatokana na mazao ya bahari, na hivyo Serikali zote mbili zitahakikisha zinaweka mkazo wa kutosha katika upatikanaji rasilimali fedha za usimamizi wa miradi.
“Tuna mikataba mbalimbali ya masuala ya mazingira ikiwemo Basel, Nairobi na mingineyo ambayo ni vyema sasa kuhakikisha Watalaamu wetu wanaangalia namna bora ya kuhakikisha rasilimali za bahari zinawanufaisha wananchi” amesema Dkt. Muyungi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Bi. Maryam Juma Abdalla amemshukuru Dkt. Muyungi kwa ziara hiyo ya kikazi na kuongeza kuwa Ofisi yake ipo tayari kuimairisha mashirikiano yaliyopo kwa manufaa ya Serikali zote mbili.
Akizungumzia miradi ya mazingira, Bi. Maryam amemuomba Dkt. Muyungi kuziomba taasisi za kimataifa kuipata fedha za kutosha na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuweza kutekeleza miradi ya mabadilkiko ya tabianchi ambayo kwa sasa yameanza kuleta athari mbalimbali.
“Hapa Zanzibar hususani maeneo ya Pemba kuna athari za wazi za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinazidi kuongezeka ikiwemo kina cha bahari na kuingia kwa maji ya bahari katika makazi ya wananchi” amesema Bi. Maryam.




