Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimepanga kuimarisha mashirikiano ili kuhakikisha fursa za Muungano zinawanufaisha wananchi na kuakisi maono ya Waasisi.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi (Januari 22, 2026) Mjini Zanzibar na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi wakati wa ziara yake aliyoifanya kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Dkt. Muyungi amesema Serikali zote mbili zimekuwa mstari wa mbele katika kutatua hoja za Muungano hatua inayolenga katika kufungua fursa za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

“Waasisi wetu walikuwa na malengo ya kubainisha fursa za mashirikiano ziweze kuwanufaisha wananchi, hivyo wakati umefika sasa wa kuhakikisha fursa hizo zinakuwa agenda muhimu tunazopaswa kuzibeba kama Watendaji wa Serikali” amesema Dkt. Muyungi.

Ameeleza kuwa ni wakati mwafaka wa kuenzi kwa matendo maono ya viongozi na waasisi wa Muungano kwa kuhakikisha wananchi wa pande zote mbili wananufaika ipasavyo kwa kufanya hivyo kutafsiri nia na malengo ya waasisi.

“Hadi sasa hoja 22 za Muungano zimepatiwa ufumbuzi, tumebaki na hoja 3 sawa na mafanikio ya asilimia 99 ya utatuzi wa hoja….ni muhimu kuhakikisha kuwa utatuzi wa hoja hizo unaleta manufaa endelevu kwa wananchi” amesema Dkt. Muyungi.

Aidha Dkt. Muyungi ameshauri kurejeshwa kwa mashindano ya michezo ya pasaka ambayo hapo awali yalikuwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha mahusiano na mashiriano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akifafanua zaidi Dkt. Muyungi amesema viongozi na watendaji wa serikali zote mbili wamekusudia kutangaza fursa za muungano kwa wananchi na kuwahimiza wataalamu kuchakata fursa hizo ili kuona njia bora ya kuwanufaisha wananchi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapnduzi Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum Ofisi hizo zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika kuimarisha uratibu wa masuala ya Muungano na hatua hiyo imeendelea kuwanufaisha wananchi wa pande zote mbili.

“Katika kikao baina yetu tumekubaliana kuimarisha mashirikiano kupitia vikao vya pamoja na tumepanga wataalamu wetu kuweza kukutana ili kuandaa maazimio na kuangalia namna bora zaidi ya kuimarisha Muungano” amesema Dkt. Islam.