Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Hatimaye wananchi waliokuwa wakihofia gharama kubwa za matibabu wanaanza kuona mwanga, baada ya Serikali kutangaza kuanza kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, mpango unaolenga kulinda haki ya msingi ya kila Mtanzania kupata huduma za afya bila kuathiriwa na uwezo wake wa kifedha.

Awamu hii ya kwanza inalenga moja kwa moja makundi yaliyo hatarini zaidi, wakiwemo wazee, watoto, wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao gharama zao za huduma za afya zitagharamiwa kikamilifu na Serikali, hatua inayotarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa kifedha kwa familia nyingi.

Katika utekelezaji wake, Serikali imeanza rasmi matumizi ya Kitita cha Huduma Muhimu chenye thamani ya shilingi 150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, huku makundi yasiyo na uwezo yakipata huduma hizo bila kulipa chochote.

Mpango huu unalenga kuhakikisha hakuna mwananchi anayekosa matibabu kutokana na ukosefu wa fedha.

Akizungumza leo, Januari 23, 2026 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema huduma hizo zitaanza kupatikana rasmi katika vituo vya afya vilivyosajiliwa kuanzia Januari 26, 2026, kwa kuzingatia mfumo wa rufaa.

Mchengerwa amesisitiza kuwa afya ni msingi wa maendeleo ya Taifa, akieleza kuwa hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kudumu endapo wananchi hawana afya njema.

Ameongeza kuwa Bima ya Afya kwa Wote ni uwekezaji wa kimkakati katika utu wa Mtanzania na ustawi wa uchumi wa nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Grace Magembe, amesema utekelezaji wa mpango huo ni hatua ya kihistoria inayobadilisha mtazamo wa huduma za afya kutoka kuwa jukumu la mtu binafsi hadi kuwa dhamana ya Taifa.

Amebainisha kuwa awamu ya kwanza inalenga kulinda makundi maalum dhidi ya gharama za matibabu zinazoweza kuwasukuma katika umaskini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, John Jingu, amesema mafanikio ya Bima ya Afya kwa Wote yatategemea kwa kiasi kikubwa uelewa na ushiriki wa wananchi.

Ameeleza kuwa wataalam wa maendeleo ya jamii wana wajibu wa kujenga mtazamo chanya na kuhamasisha jamii ili mpango huo uwe suluhu ya kudumu ya changamoto ya gharama za matibabu na kichocheo cha ustawi wa jamii.