Na Mwandishi wetu, Simanjiro

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mwalimu Fakii Raphael Lulandana ameeleza kwamba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeing’arisha Simanjiro kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.

DC Lulandala akizungumza mji mdogo wa Orkesumet makao makuu ya Wilaya hiyo amesema Rais Samia katika kipindi kifupi cha utawala wake amefanikisha maendeleo mengi katika eneo hilo.

Ameeleza kwamba kwenye sekta ya nishati ya umeme hivi sasa vijijini vyote 56 vya Wilaya ya Simanjiro vina huduma hiyo ikibakia vitongoji vichache ambavyo navyo vitafungiwa umeme.

“Wakati Rais Samia anaingia madarakani katika Wilaya ya Simanjiro ni vijiji 21 pekee ambavyo wananchi wake walikuwa wanapata nishati ya umeme,” ameeleza DC Lulandala.

Amesema hata baadhi ya watu wa Simanjiro waliodanganywa na baadhi ya wanasiasa kuwa maeneo yao yataporwa na kugeuzwa kuwa mapori tengefu na mapori ya akiba niliwaeleza wasiamini hayo.

“Rais Samia hawezi kuwanyang’anya ardhi kisha awaletee maendeleo, sasa ataleta umeme ili tembo au fisi watumie badala ya watu, leo hii ndiyo wengine wanaamini tulivyosema,” amesema DC Lulandala.

Amesema kwa upande wa sekta ya afya, wakati Rais Samia akiingia madarakani Wilaya ya Simanjiro ilikuwa na vituo vitatu pekee vya afya ila hivi sasa kuna vituo nane.

“Kulikuwa na vituo vitatu vya Orkesumet, Mirerani na Naberera ila hivi sasa vimeongezeka vingine vitano na kufikisha idadi ya vituo nane vya afya ambavyo vimesogeza huduma ya afya kwa karibu na jamii,” amesema DC Lulandala.

Amesema hata katika sekta ya maji Simanjiro imepiga hatua kubwa kwani japokuwa hayatoshi ila watu na mifugo hawaangaiki tena kama awali.

“Pia Raisi Samia ametupa heshima kubwa wana Simanjiro na tunamshukuru sana kwani mbunge wetu mhe James Ole Millya amemteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,” amesema DC Lulandala.
Ameongeza kwamba hata katika sekta ya elimu shule nyingi za msingi na sekondari zimejengwa Simanjiro ili kuongeza wasomi.

Amesema kutokana na maendeleo hayo yaliyofanyika ndiyo sababu wana Simanjiro na Watanzania kwa ujumla wakampa kura nyingi za kutosha Rais Samia ili aendelee kuwaongoza kwa upendo na kuzidi kuwaletea maendeleo.