Na Mwandishi Wetu
Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya dhati katika kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuweka mikakati madhubuti itakayowainua kutoka kwenye uchuuzi wa mitaani na kuwa wazalishaji wakubwa na wamiliki wa biashara endelevu.
Kupitia mpango wa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi kwa Vijana (Youth Special Economic Zones), serikali inalenga kusaidia uanzishwaji wa kampuni zisizopungua 20,000 za vijana ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, hususan katika sekta za kilimo, ufugaji na viwanda, hatua itakayochochea ajira na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza awali na viongozi wa Mkoa wa Kagera katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, alisema mkakati huo unalenga kuwabadilisha vijana kutoka kwenye biashara ndogondogo zisizo rasmi na kuwajengea uwezo wa kuwa wawekezaji wakubwa wa baadaye.
“Lengo letu ni kuona vijana wanamiliki uchumi, wanazalisha, wanaajiri wengine na siyo kubaki kwenye uchuuzi wa muda mfupi,” alisema Nanauka.
Katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Kagera, Mhe. Nanauka alitembelea miradi mbalimbali inayosimamiwa na vijana katika Wilaya za Muleba, Missenyi, Karagwe na Manispaa ya Bukoba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kujionea utekelezaji wa sera za maendeleo ya vijana kwa vitendo.
Moja ya miradi iliyomvutia zaidi ni mradi wa ufyatuaji wa tofali unaomilikiwa na kikundi cha Umoja wa Vijana Business kilichopo Wilaya ya Muleba. Akiwa katika eneo hilo tarehe 24 Januari 2026, Waziri alijionea shughuli za uzalishaji na kusikiliza maelezo ya kina kuhusu mafanikio, changamoto na mipango ya baadaye ya vijana hao.
Mhe. Nanauka aliwapongeza vijana hao kwa ubunifu na bidii, akibainisha kuwa mradi huo ni mfano halisi wa namna vijana wanavyoweza kujiajiri na kujiletea maendeleo bila kusubiri ajira za kuandikishwa.
Aidha, alitoa wito kwa vijana wote nchini kutumia kikamilifu mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na serikali kupitia Halmashauri zao, akisisitiza kuwa mikopo hiyo ni fursa muhimu ya kuanzisha na kukuza miradi ya kiuchumi.
Kwa upande wao, vijana wa Umoja wa Vijana Business waliishukuru serikali kwa kuweka mazingira wezeshi, wakieleza kuwa mikopo, mafunzo na ushirikiano kutoka taasisi za umma umekuwa chachu ya mafanikio yao. Waliahidi kuongeza juhudi ili kupanua uzalishaji, kuongeza ajira kwa vijana wenzao na kuchangia pato la jamii inayowazunguka.
Kwa ujumla, ziara ya Mhe. Nanauka mkoani Kagera imeonesha kwa vitendo mwelekeo mpya wa sera za maendeleo ya vijana nchini – sera zinazoweka mkazo kwenye uzalishaji, ubunifu na umiliki wa uchumi badala ya utegemezi na uchuuzi wa muda mfupi.











