
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu, amekutana na mwanamuziki mashuhuri nchini Comoro, Samra Athoumani maarufu kama “La Diva”, ambaye alitembelea Ubalozi wa Tanzania ili kuelezea azma yake ya kushirikiana na ubalozi katika kuhimiza utunzaji wa mazingira kupitia taasisi yake ya Twamaya.
Katika mazungumzo hayo, La Diva alimueleza Balozi Yakubu kuwa taasisi ya Twamaya inalenga kuendesha tukio kubwa la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuimarisha mfuko wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira nchini Comoro. Aidha, alieleza kuwa anakaribisha ushiriki wa taasisi na wadau kutoka Tanzania katika tukio hilo, kwa lengo la kuongeza nguvu na ufanisi wa kampeni za uhifadhi wa mazingira.
La Diva pia alibainisha kuwa yeye ni miongoni mwa wasanii wa kwanza nje ya Tanzania kutunga nyimbo za kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2021, hatua ambayo inaonesha upendo na mshikamano wake na Tanzania.
Kwa upande wake, Balozi Yakubu alimpongeza La Diva kwa kutumia sanaa kama chombo chenye ushawishi mkubwa katika kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya maendeleo, hususan utunzaji wa mazingira. Balozi Yakubu aliahidi kulifanyia kazi ombi la ushirikiano huo kwa kushirikisha wadau husika kutoka Tanzania, ili kuona namna bora ya kuunga mkono juhudi za taasisi ya Twamaya na kuimarisha ushirikiano wa kijamii na kimazingira kati ya Tanzania na Comoro.




