Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Nzega
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kupitia mkandarasi wake, WASCO ISOAF Tanzania Limited umekabidhi miundombinu ya vyoo vya kisasa na madarasa kwa Shule za Msingi na Sekondari za Igusule, zilizopo Kijiji cha Sojo, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kurudisha kwa jamii (CSR).
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya miundombinu hiyo, Mkurugenzi wa Mradi wa WASCO ISOAF, Bw. Gary Deason, alisema lengo msaada huo ni kuhakikisha jamii zinazozunguka mradi huo zinanufaika moja kwa moja na uwepo wa mradi huo, hususan katika sekta za maendeleo ikiwemo elimu.

Bw. Deason alisema kuwa ushirikiano walioupata kutoka kwa wananchi wakati wa utekelezaji wa shughuli za mradi umekuwa nguzo muhimu katika kufanikisha hatua hii.
“Napenda kuishukuru EACOP kwa dhamira yake endelevu ya kuunga mkono maendeleo ya jamii sambamba na utekelezaji wa wajibu wa kisheria wa wakandarasi kurudisha kwa jamii (CSR),” alisema Bw. Deason.
Aliongeza kuwa msaada huo wa kusaidia jamii unaojulikana kama ‘Maendeleo Program’, umelenga kuacha athari chanya kwa jamii zinazozunguka Kiwanda cha Mfumo wa Ukingaji Joto (Thermal Insulation System – TIS) kilichopo Sojo, katika kata hiyo ya Isugule yenye vijiji saba.
Mbali na miradi hiyo, kampuni hiyo pia mwaka 2024 ilisimamia na kukabidhi ujenzi wa madarasa mawili katika Kijiji cha Selemi, kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kijiji katika Kijiji cha Ilalo, pamoja na kutoa msaada wa samani za shule na ofisi, zikiwemo madawati 108, viti nane, meza nane na makabati matatu kwa Shule ya Msingi Wella II.
Lakini pia ilidhamini vijana 194 kupata mafunzo ya ufundi stadi katika fani mbalimbali na kunufaika na bima ya afya kwa mwaka mmoja, kulipiwa vifaa vya masomo, posho na mahitaji mengine muhimu.

Aidha, kampuni hiyo imeajiri wafanyakazi 760, wakiwemo wenye ujuzi maalum, ambapo 310 kati yao walitoka katika vijiji vya Kata ya Igusule.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Bi. Zaina Ayubu Dikolagwa, alisema kuwa mchango wa WASCO ISOAF chini ya mradi wa EACOP ni mfano wa kuigwa na kuzitaka kampuni nyingine kutekeleza wajibu wao wa kisheria, ikiwemo kuzingatia sheria ya maudhui ya ndani (Local Content).
“Uwepo wa mradi wa EACOP wilayani kwetu umeleta manufaa makubwa kwa jamii na kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali, ikiwemo elimu,” alisema Bi. Zaina.
Kwa upande wa EACOP, Bw. Adonis Kimbembe, Meneja anayesimamia kiwanda hicho cha EACOP alisema kuwa uwekezaji katika jamii ni nguzo muhimu ya mradi huo, mbali na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji mafuta ghafi.

“Ushirikiano wetu na WASCO ISOAF unaakisi dhamira pana ya EACOP ya maendeleo yenye uwajibikaji kwa jamii kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu” alisema Bw.Kimbembe.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Igusule, Bw. Eliud Douglas, alishukuru kwa msaada huo akisema umeondoa changamoto kubwa ya upungufu wa huduma za vyoo shuleni hapo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Binti. Zainab Mihambo, mwanafunzi wa Kidato cha Nne, alisema kuwa ujenzi wa vyoo vya kisasa utachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi, hususan wa kike, ambao hapo awali walikosa kuhudhuria masomo wakati wa kipindi cha hedhi kutokana na miundombinu duni, ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama.
Bomba la EACOP, lenye urefu wa kilometa 1443, linaanzia Wilaya ya Hoima nchini Uganda na kuishia nchini Tanzania katika Mkoa wa Tanga na limepita katika mikoa nane ya Tanzania bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
Wanahisa wa EACOP ni TotalEnergies yenye asilimia (62), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) yakimiliki asilimia 15 kila moja na kampuni ya mafuta ya Kichina (CNOOC) ikiwa na asilimia nane.




