Na Munir Shemweta, WANMM
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeingilia kati mgogoro wa matumizi ya ardhi unaomhusisha mwekezaji Rashid Kwanzibwa, aliyedaiwa kubomoa baadhi ya majengo yaliyokuwa kwenye maeneo ya serikali na kuanzisha miradi bila utaratibu katika eneo la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, Geita.
Akitolea ufafanuzi kuhusu suala hilo leo, tarehe 26 Januari, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema wizara yake inaungana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha mgogoro unafanyiwa kazi na kukamilika.
Mhe. Dkt Akwilapo amewakumbusha wamiliki wa maeneo yote nchini kuzingatia matumizi yaliyokusudiwa katika hati miliki zao, na endapo mmiliki ana mpango wa kuendeleza eneo lake kwa matumizi tofauti na yaliyotolewa katika hati, ni lazima apate kibali cha mabadiliko ya matumizi kama sheria inavyoelekeza.
”Hatua hiyo itahakikisha maeneo yanaendelezwa kwa kuzingatia mpango, na hivyo kuondoa migongano ya matumizi, kutunza mazingira, na kuweka nadhifu miji yetu”. Amesema
Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, uendelezaji wowote unaofanyika sharti uzingatie sheria za uendelezaji miji, ikiwa ni pamoja na kupata vibali vyote vinavyotolewa na mamlaka zote za serikali. Kwa sasa, wataalamu wa Wizara wameungana na TAMISEMI kushughulikia suala hilo, na baada ya uchunguzi kukamilika, kutatolewa taarifa rasmi ya pamoja.
Uamuzi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuingilia kati sakata hilo unafuatia kusambaa kwa picha mjengeo katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ikionesha Kamati ya Fedha na Uchumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikilazimika kusimamisha shughuli za mradi wa ujenzi wa vibanda vya maduka kwenye eneo la viwanja vya CCM Katoro, huku ikidaiwa mwekezaji kuingia mipaka ya serikali ya kijiji katika Kitongoji cha Katoro Center kilichopo mji mdogo wa Katoro mkoani Geita.


