Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MKOA wa Pwani unaunga mkono dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendeleza agenda ya uhifadhi wa mazingira kwa kugawa miche ya mikorosho milioni 1.5 kwa wakulima wa Wilaya ya Rufiji.
Aidha, mkoa huo utaendesha zoezi la upandaji wa miti 6,379, ikiwemo miti 671 ya matunda na miti 5,708 ya mbao na vivuli, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayotarajiwa kuadhimishwa Januari 27, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alisema zoezi hilo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi na maono ya Serikali katika kulinda na kutunza mazingira, hususan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kunenge alieleza kuwa, jumla ya miti itakayopandwa mkoani Pwani ni milioni 13.5, ambapo kila Halmashauri kati ya tisa zilizopo mkoani humo inatarajiwa kupanda miti milioni 1.5 wakati wa msimu wa mvua za masika.
Alieleza miti 6,379 itakayopandwa katika zoezi la maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais itapandwa katika maeneo ya shule, ambapo wanafunzi watashiriki katika kuitunza ili kuwajengea uzalendo na uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
“Kaulimbiu yetu ni Uzalendo ,kutunza mazingira, shiriki kupanda miti,” alisema Kunenge.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji miti ili kulinda mazingira na kuimarisha ustawi wa jamii.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa Januari 27, 2026 kwa kuongoza zoezi la upandaji miti katika maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi, Zanzibar, akitimiza miaka 66 tangu kuzaliwa mwaka 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.


