Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

MWANAMKE mmoja Catherine Kinyongile (56) mkazi wa kijiji cha Ndonga kilichopo katika Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma amefariki dunia baada ya kukamatwa na mamba wakati akioga katika eneo la fukwe la forodha ya Hyetu iliyopo ziwa Nyasa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu, majira ya saa 4 usiku, huko katika kijiji cha ndonga kata Liwundi Tarafa ya Ruhuhu ambako inadaiwa mwanamke aliyetambulika kwa jina la Catherine alifariki dunia baada ya kukamatwa na mamba wakati akioga kandokando ya Ziwa Nyasa.

Kamanda Chilya alifafanua kuwa Catherine akiwa na mtoto wake wa kike aitwae Josepha Kibena (30) walienda katika fukwe hizo zilizopo umbali wa mita 50 toka kwenye nyumba yao wanayoishi na Catherine aliingia majini kwa ajili ya kuoga ndipo mamba alipomvamia na kumkamata na kumzamisha ziwani.

Alisema baada ya Josepha kuona tukio hilo la kukamatwa mama yake mzazi na mamba alipiga kelele huku akilia kuita watu kwa kuomba msaada ndipo wananchi walifika eneo la tukio na kuanza kumtafuta na ilipofika majira ya saa 8 usiku walifanikiwa kumpata mama huyo akiwa mahututi akielea majini huku mwili wake ukiwa umejeruhiwa vibaya tumboni na mkono wa kulia ambapo mama huyo alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitali kutokana na kuvuja damu nyingi.