Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Unguja
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, amesema uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeiwezesha nchi kupiga hatua kubwa katika uhifadhi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuimarisha Muungano, kwa misingi ya maendeleo endelevu.
Mhe. Masauni ameyasema hayo katika hafla ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyofanyika Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja, Januari 27,2026 ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia aliongoza zoezi la kupanda miti.
Amesema Rais Mhe. Dkt. Samia ameiongoza Tanzania kufanya mageuzi makubwa ya kimkakati katika sekta ya mazingira, ikiwemo kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kufikia zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Amesema Rais Mhe. Dkt. Samia ameongoza juhudi za kimataifa za kutafuta rasilimali za kifedha kwa ajili ya nishati safi ya kupikia barani Afrika, hatua iliyoongeza nafasi ya Tanzania kunufaika na mifumo ya ufadhili wa kimataifa katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema hatua hiyo imechangia Rais kutambuliwa kitaifa na kimataifa kama kiongozi mahiri anayelipa kipaumbele suala la mazingira.

“Chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia, Tanzania imeanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni, hatua inayoiwezesha nchi kunufaika zaidi na fursa za soko la biashara ya kaboni sambamba na kuongeza mapato yatokanayo na uhifadhi wa mazingira,” amesema Mhe. Masauni.
“Fedha za mazingira na mabadiliko ya tabianchi zimeongezeka kupitia vyanzo vya ndani na nje, sambamba na kuanzishwa kwa Kitengo Maalum cha Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi,”
Ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania imepata Dira ya Taifa ya Maendeleo inayotambua mazingira na uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kama nguzo mahsusi ya maendeleo, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2025–2030) yenye vipaumbele vinavyolenga uhifadhi wa mazingira.
Kuhusu Muungano, Waziri Masauni amesema Rais Samia amewezesha kutatuliwa zaidi ya hoja 15 kati ya hoja 18 za Muungano alizozikuta, hatua iliyosaidia kuimarisha mshikamano, amani na utulivu kati ya pande mbili za Muungano.
Vilevile ameiongoza nchi kuandaa Sera ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 inayolenga kuimarisha sekta za uchumi wa buluu kwa misingi ya uendelevu, ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Mhe. Masauni amewahamasisha Watanzania kuiga mfano wa RaisMhe. Dkt. Samia kwa kuadhimisha matukio muhimu ya maisha yao kwa kupanda miti na kuhakikisha miti hiyo inatunzwa hadi kukua, endapo watu milioni 30 wangepanda mti mmoja kila mmoja katika siku zao za kuzaliwa, taifa lingeongeza angalau miti milioni 30 kila mwaka, hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.



