Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
KATIKA kuadhimisha siku ya kumbukizi ya kuzaliwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,
rai imetolewa kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa wito huo ameutoa leo Januari 27, mkoani Dodoma wakati wa zoezi la upandaji miti katika Skimu ya Umwagiliaji Hombolo, lililoendeshwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Senyamule amesisitiza matumizi endelevu ya rasilimali za maji, na usimamizi shirikishi wa miundombinu ya umwagiliaji, ili kuongeza ufanisi na uimara wa miradi hii.
“Serikali ya Mkoa wa Dodoma itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji pamoja na wadau wote wa maendeleo katika kuhakikisha kuwa miradi ya umwagiliaji inatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi bora ya uhifadhi wa mazingira, sambamba na kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Senyamule amewahimiza wananchi wote kushiriki kikamilifu katika juhudi za kupambana na uharibifu wa mazingira kwa kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji na kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Amesisitiza kuwa kaulimbiu ya “Umwagiliaji, Kilimo cha Uhakika” haitaweza kufikiwa bila mazingira salama na rasilimali za maji zinazolindwa ipasavyo.
Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa amesema miti 1,000 aina ya mzambarau imepandwa huku akisisitiza
hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mipango ya Usimamizi wa Mazingira na Jamii iliyoandaliwa na Tume kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji nchini.
“Kadhalika hatua hii inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuunganisha maendeleo ya kilimo na uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.”amesema.
Amebainisha kuwa upandaji wa miti rafiki ya maji, hususan katika vyanzo vya maji kama Bwawa la Hombolo, ni hatua ya kimkakati inayolenga kulinda rasilimali za maji, kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji ya umwagiliaji.
Pia, kupunguza athari za mmomonyoko wa udongo, pamoja na kuimarisha ikolojia ya eneo hili muhimu kwa uzalishaji wa chakula na maendeleo ya wakulima.





