Na Mwandishi Wetu

VIJANA Jijini Dar es Salaam wameungana kusherehekea siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, wakitumia fursa hiyo kupongeza mafanikio ya Serikali katika kuwafungua kiuchumi na kielimu ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Maadhimisho hayo yalifanyika leo Januari 27, 2026, yakiratibiwa na Taasisi ya Together for Samia, huku yakihusisha vijana kutoka makundi na taasisi mbalimbali waliokusanyika kuonesha mshikamano wao na kuunga mkono uongozi wa Rais Samia.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mratibu wa Taasisi ya Together for Samia, Gulatone Masiga, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya mageuzi makubwa yaliyowanufaisha moja kwa moja vijana, hususan katika sekta za elimu, ujuzi, ajira na uwezeshaji wa kiuchumi.

Masiga amesema miongoni mwa mafanikio makubwa ya Rais Samia ni ujenzi wa vyuo vya ufundi na ujuzi katika zaidi ya wilaya 62 nchini, hali iliyofungua fursa kwa maelfu ya vijana kupata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri na kushindana katika soko la ajira.

“Rais Samia amewekeza kwa vitendo kwenye kizazi cha sasa na kijacho. Vyuo hivi vya ufundi vimekuwa chachu ya kuwapa vijana ujuzi unaohitajika katika dunia ya sasa,” amesema Masiga.

Ameongeza kuwa Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuanzisha mtaala mpya unaolenga kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari wanakuwa na stadi za kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Aidha, Masiga amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya nishati umechangia kuchochea ukuaji wa viwanda, biashara na uwekezaji, hatua iliyoongeza ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana.

Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana Innovations, Dorcas Mshiu, amesema ameungana na vijana wengine kuadhimisha siku hiyo ya kumbukizi kwa kutambua mchango mkubwa wa Rais Samia katika kufungua mazingira rafiki ya biashara kwa vijana.

Mshiu amesema kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, vijana wengi wameanza kusajili biashara zao rasmi, hali inayoonesha kufunguka kwa mazingira ya kibiashara na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa ndani na nje.

“Hii ni ishara kwamba nchi imefunguka kiuchumi na vijana wamepewa nafasi ya kuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa,” amesema.

Ameongeza kuwa mkakati wa Serikali wa mikopo yenye riba ya asilimia nne kwa vijana umekuwa msaada mkubwa kwa vijana wanaojishughulisha na ujasiriamali na kujiajiri.

“Mikopo hii imewawezesha vijana wengi kufungua na kukuza biashara, kuongeza kipato na kujikwamua kimaisha,” amesema Mshiu.

Naye mshiriki wa maadhimisho hayo, Nathaniel Maseke, amesema vijana wanaendelea kumuombea Rais Samia ili aendelee kuwaongoza Watanzania kwa misingi ya umoja, mshikamano na bidii katika kazi.

“Tunaamini kupitia uongozi wake, vijana wataendelea kuhamasishwa kushikamana, kufanya kazi kwa bidii na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa,” amesema Maseke.

Maadhimisho hayo yametumika kama jukwaa la vijana na viongozi mbalimbali kutafakari safari ya uongozi wa Rais Samia na mchango wake katika kulijenga Taifa lenye fursa, mshikamano na matumaini kwa kizazi cha sasa na kijacho.