Na Mwandishi Wetu, JammhuriMedia, Tanga
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la watoa huduma za hifadhi ya jamii, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Tuzo hiyo imekabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, kwa Meneja wa NSSF Mkoa wa Tanga, Nuhu Mbaga, katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yameandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha, kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ikiwemo NSSF.

Kupitia ushiriki wake, NSSF iliendelea kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi, kuandikisha wanachama wapya, na kuhamasisha wanachama waliopo kutumia mifumo ya kidijitali kupata huduma mbalimbali.
Mifumo hiyo ni pamoja na NSSF Portal, NSSF App na huduma ya USSD (15200#), inayowawezesha wanachama kupata taarifa za michango yao, kutengeneza namba za kumbukumbu za malipo (Control Number), kulipia michango, pamoja na kufungua madai ya mafao kwa njia ya mtandao.





