Madaktari katika hospitali ya Alert huko Addis Ababa wamefanikiwa kurudisha uume uliokatwa wa kijana mmoja baada ya upasuaji wa saa saba.
Dkt. Abdurrezak Ali, mkuu wa Idara ya Upasuaji na Urekebishaji, aliambia BBC kwamba mgonjwa huyo alijiumiza usiku wa manane Jumamosi, Januari 24, 2026.
Alipelekwa kwanza kwenye kliniki ya eneo, ambayo baadaye iliwasiliana na hospitali ya Alert kuuliza ikiwa kuunganishwa tena kwa uume kuliwezekana.
“Tulifanya uamuzi wa kufanya upasuaji kwa sababu tuliamini kwamba uume bado unaweza kuunganishwa tena, kulingana na muda uliopita tangu kukatwa,” Dk. Abdurrezak alieleza.
Uume ulikuwa umekatwa kabisa, na kuuacha bila mzunguko wa damu au oksijeni kwa muda wa saa tisa. Hata hivyo, Dk. Abdurrezak alibainisha kuwa mgonjwa huyo hakuwa akivuja damu nyingi, maumivu yake yalikuwa kidogo, na hali yake haikuwa mbaya sana alipolazwa.
Sehemu ya sentimita tano ya uume ilikuwa imehifadhiwa katika hali ya baridi, ambayo iliongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha kufanikiwa kwa upasuaji huo.
Madaktari wa upasuaji waliunganisha tena mishipa ya damu na neva, wakarekebisha miundo ya njia ya mkojo, na kurejesha tishu husika.
“Utafiti unaonyesha kwamba neva na mishipa ya damu inaweza kuishi hadi saa 16 baada ya kukatwa kwa sababu hakuna misuli katika uume. Katika hali hiyo, uume uliweza kuunganishwa upya baada ya saa tisa,” Dk Abdurrezak alisema.
Mgonjwa, katika ujana wake, sasa anapata nafuu. Madaktari wanatarajia aanze kukojoa kawaida ndani ya wiki tatu, wakati uwezo wa kufanya ngono inaweza kuchukua takriban miezi mitatu.
“Haruhusiwi kufanya mapenzi katika kipindi hiki, kwani inaweza kuharibu urekebishaji wa neva,” Dk. Abdurrezak aliongeza.

