Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha maeneo ya wazi yaliyopo katika mitaa na kata mbalimbali hayauzwi, bali yaachwe kwa ajili ya mazoezi na shughuli za michezo kwa vijana.

Ameyasema hayo bungeni Dodoma, akijibu swali la Mbunge Abdul Yusuf Maalim (Jimbo la Amani) kuhusu mikakati ya Serikali ya kukuza michezo kuanzia ngazi za shule. Dkt. Mwigulu alisema kuwa maeneo ya wazi ni muhimu katika kuibua vipaji, kuandaa timu bora, na kuongeza uwezekano wa nchi kushiriki vizuri kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa. Pia aliongeza kuwa utunzaji wa maeneo haya utasaidia kuhakikisha mazingira bora ya mazoezi yanapatikana na kuongeza idadi ya vijana wanaojihusisha na michezo.

Aidha, Waziri Mkuu alibainisha hatua za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo kutenga shule 56 nchini kuwa maalum kwa mafunzo ya vipaji vya michezo, kuongeza mashindano ya shule za msingi kupitia UMITASHUMTA, na mashindano ya shule za sekondari kupitia UMISSETA, sambamba na kuimarisha mashindano yanayodhaminiwa na taasisi za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Serikali pia imeendeleza viwanja vya mazoezi vilivyopo mikoani, kujenga vipya, na kuboresha viwanja vinavyotumika kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa ikiwemo AFCON. Dkt. Mwigulu alisisitiza mfano wa baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa walioanza katika maeneo ya wazi, akibainisha kuwa maeneo hayo ni kiungo muhimu cha kukuza vipaji vya michezo nchini.

Serikali inasisitiza kuwa michezo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya jamii na vijana na inawataka wadau wote kushirikiana kuhakikisha maeneo ya mazoezi yanatunzwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.