Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa vitendo kupitia mikopo yenye masharti nafuu.
Amesema kuwa mikopo hiyo inatolewa kupitia Benki ya NMB ambayo imeingia makubaliano na Serikali kusimamia mikopo hiyo, ikiwa na riba ya asilimia saba (7%) kwa mwaka.
Aidha amebainisha kuwa mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo wenye mauzo ghafi yasiyozidi Shilingi Milioni Nne (4,000,000) kwa mwaka, wakiwemo mama na baba lishe, machinga, waendesha bodaboda wa magurudumu mawili, matatu na guta pamoja na makundi mengine yanayotambuliwa na kusajiliwa na Mamlaka husika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Gwajima amesema kuwa ili mfanyabiashara ndogondogo aweze kunufaika na mikopo hiyo anatakiwa awe ametambuliwa na kusajiliwa kwenye Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBN–MIS) na Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Halmashauri yake.
Aidha ameongeza kuwa mfanyabiashara anatakiwa awe raia wa Tanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18, awe na biashara inayotambuliwa katika eneo lake au eneo linalotambuliwa na Mamlaka husika pamoja na kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au Namba ya NIDA.
Amesema kuwa utaratibu wa kuomba mikopo hiyo ni wazi na rafiki ambapo mwombaji mwenye kitambulisho cha kidijitali au namba ya kitambulisho hicho anatakiwa kufika katika Benki ya NMB kwa ajili ya kujaza fomu ya maombi na kuwasilisha nyaraka zinazohitajika.
Aidha amebainisha kuwa maombi yote yanahakikiwa na kuchambuliwa kwa mujibu wa taratibu za benki hiyo na waombaji wanaokidhi vigezo wanaingiziwa fedha kwenye akaunti zao kulingana na aina ya mkopo waliyoomba.
Ameongeza kuwa mikopo hiyo ina masharti nafuu ikilinganishwa na mikopo ya kibiashara, ambapo muda wa mkopo ni kuanzia miezi mitatu (3) hadi miezi ishirini na minne (24) kulingana na aina ya biashara.
Aidha amebainisha kuwa riba ya mkopo huo ni asilimia 7% kwa mwaka na mkopo umewekewa bima dhidi ya kifo na ulemavu wa kudumu kwa mkopaji kwa lengo la kumlinda mfanyabiashara na familia yake.
Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali inawahamasisha wafanyabiashara ndogondogo kuchangamkia fursa hiyo kwa wingi kwani ni sehemu ya mkakati wa kuongeza mitaji, kukuza biashara, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kukuza uchumi jumuishi kwa Taifa kwa ujumla.
Aidha ameongeza kuwa wafanyabiashara ambao bado hawajatambuliwa na kusajiliwa kwenye mfumo wa WBN–MIS wanahimizwa kufika katika Ofisi za Kata au Halmashauri za Wilaya walipo ili kukamilisha zoezi la utambuzi na usajili.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Benki ya NMB kuhakikisha mikopo hiyo inawafikia walengwa kwa uwazi, haki na kwa wakati huku ikisisitiza nidhamu ya marejesho ya mikopo ili fursa hiyo iwanufaishe wananchi wengi zaidi.
Pia, amebainisha kuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum itaendelea kusimamia na kuboresha mifumo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa lengo la kujenga Taifa lenye usawa, fursa na ustawi kwa wote.


