Wanandoa wawili nchini Indonesia wamepigwa viboko mara 140 kwa kufanya mapenzi nje ya ndoa ambayo ni makosa au haram katika sheria za dini ya kiislamu.

Mwanaume na mwanamke hao walipigwa viboko hivyo hadharani.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 21, alizirai baada ya kupigwa viboko hivyo katika wilaya ya Aceh.

Maafisa watatu wa polisi walimpiga viboko kwa zamu mwanamke huyo, aliyekuwa akilia kwa maumivu.

Baada ya kuzirai, polisi walimsafirisha kwa kutumia ambulensi na kumuondoa katika eneo hilo.

Wawili hao walaidhibiwa siku ya Alhamishi pamoja na wengine wanne ikiwemo afisa mmoja wa polisi na mchumba wake ambao walipigwa viboko 23, baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja sheria za dini ya Kiislamu maarufu Sharia.

Kupigwa viboko ni moja ya adhabu ambazo hupewa mtu anayevunja sheria za dini ya kiislamu katika wilaya ya Aceh, nchini Indonesia, ingawa adhabu hiyo inakoselewa sana kutokana na ukatili wake.

Katika sheria za dini ya Kiislamu wilaya ya Aceh, kufanya mapenzi nje ya ndoa, mtu hupewa adhabu ya viboko 100, na viboko 40 kwa kunywa pombe.

Wilaya ya Aceh, ndiyo wilaya pekee nchini Indonesia ambayo inashurutisha utiifu wa sheria za dini ya kiislamu na huwaadhibu wanaovunja sheria hizo kwa kuwapiga viboko mbele ya umati wa watu.