Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Msimamizi wa mifumo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Pwani, Kenneth Mnnembuka, ametoa wito kwa taasisi na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha zinatekeleza matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kutenga na kutoa kwa uwazi asilimia 30 ya zabuni kwa vikundi maalum vinavyohusisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa matakwa hayo haupaswi kubaki kwenye maandishi ya sera pekee, bali uonekane kwa vitendo kupitia tenda zinazotangazwa, mikataba inayotolewa na taarifa za utekelezaji zinazoeleweka kwa umma.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa kwa lengo la kuwawezesha wadau wa ununuzi kushiriki katika tenda za serikali, Mnnembuka amesema hatua hiyo itasaidia kuvijengea vikundi hivyo uwezo wa kiuchumi, kukuza ajira na kupunguza utegemezi.
Aidha, ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha inapaswa kutoa elimu endelevu kuhusu mfumo wa usajili wa tenda za PPRA (NeST), kurahisisha taratibu za usajili na kuhakikisha vikundi vinavyostahili havikwamishwi na urasimu usio wa lazima.
Kwa upande wake, mshiriki wa mafunzo hayo, mjasiriamali kutoka Mayo Construction Group, wanaojihusisha na uzalishaji wa tofali, anasema vikundi vingi havina uelewa wa kutosha kuhusu mfumo wa NeST, hivyo akaishauri serikali kupanua wigo wa mafunzo ili kuwafikia wadau wengi zaidi.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kukuza mitaji yao na kuongeza fursa ya kushinda tenda za serikali.
Naye mshiriki mwingine, AbdulAzizi Simulizi, Katibu wa kikundi cha Motomoto Unit, amesema kikundi hicho kimesajiliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha tangu mwaka 2024 na tayari kipo kwenye mfumo wa NeST.
Alisema iwapo vikundi havitapatiwa elimu ya kutosha, vitashindwa kunufaika na fursa ya asilimia 30 ya zabuni zilizotengwa kwa vikundi maalum.
AbdulAzizi ameishukuru serikali kupitia PPRA kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yamekuwa mkombozi kwa vikundi mbalimbali, na akaahidi wao kama wanufaika kwenda kuwaelimisha wengine ili waweze kunufaika na mfumo huo.





