Na Mwandishi wetu, Simanjiro

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamewapongeza mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) na shirika la ugavi wa nishati ya umeme (TANESCO) kwa utendaji kazi wao kwani unawapa usingizi.

Hata hivyo, madiwani hao wamezitaka taasisi nyingine zinazofanya kazi katika Wilaya hiyo ya Simanjiro kujipanga na kuona namna wanavyotekeleza wajibu wao kama RUWASA na TANESCO.

Diwani wa Kata ya Ngorika, Albert Msole akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ameeleza kuwa TANESCO na RUWASA wanastahili kupongezwa kwa namna wanavyojitoa katika kuitumikia jamii.

“RUWASA na TANESCO wanasababisha wana Simanjiro walale usingizi mwororo kwa namna wanavyofanya kazi ya kutoa huduma kwa jamii,” amesema Msole.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mwanjaa Jacob amewapongeza TANESCO kwa namna wanavyosambaza nishati ya umeme katika maeneo ambayo hayajapata.

“Niwapongeze TANESCO kwani wameweza kufunga umeme kwenye eneo la Lemshuku katika machimbo ya madini ya Tomarini ya kijani kupitia REA,” amesema Mwanjaa.

Diwani wa Kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Mardadi) amewapongeza RUWASA kwa kusambaza maji katika vijiji vyake.

Diwani wa Kata ya Ruvu Remit, Yohana Maitei (Kadogoo) amewapongeza RUWASA na kuwasihi wamalizie kuweka huduma ya maji katika taasisi za elimu.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Joanes Martin amesema watu 32,456 watanufaika na maji kupitia miradi ya thamani ya shilingi 4,013,672,243.89.

Mhandisi Joanes ameeleza kwamba kiasi hicho cha fedha kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji katika Wilaya ya Simanjiro, ambayo tayari ilishaanzishwa.