Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Nairobi

Kwa muda mrefu Jiji la Dar es Salaam limekuwa kama linaishi kwa mazoea katika suala la kusimamia biashara za wamachinga.

Si Dar es Salaam pekee, bali karibu mikoa yote ya Tanzania. Watu hawa ni nguzo muhimu ya uchumi, ndio wanaochangia ajira, kipato na mzunguko wa pesa mitaani. Hata hivyo, ni lazima tukubali kuwa hali ya wamachinga ilipofikia – hasa katika Jiji la Dar es Salaam, maeneo ya Kariakoo, Mbagala na mengine – haikustahili kukaliwa kimya. Barabara zimegeuzwa masoko, watembea kwa miguu hapapitiki, magari ndiyo usiseme, miundombinu ya usalama kama mifumo ya maji haionekani tena, kukitokea moto inashindwa kufanya kazi kutokana na msongamano usio na mpangilio.

Sitanii, nafahamu huu ni mfupa mgumu. Wamachinga wamegeuka Jimbo la Uchaguzi lisilokuwa na mipaka. Vyama vya siasa – tawala na upinzani, wamewekeza kwa wamachinga kupata kura, kwa kuwaambia wasiguswe walipo. Rais mmoja alipata kuwaambia: “Hata kwenye dirisha la ofisi ya Mkuu wa Wilaya tundika mashati yako uuze, nione anakugusa!” Tumesahau? Hapo ndipo tunapopaswa kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Hatua yake ya kuwaondoa wamachinga katika maeneo ya katikati ya Jiji na Kariakoo haikuwa kazi rahisi. Ilikuwa ni uamuzi wa kisiasa na kiutawala uliotakiwa ujasiri mkubwa. Ni wachache wanaoweza kufanya uamuzi mgumu na kujisimamia, lakini RC Chalamila ameonyesha kuwa Dar es Salaam inaweza kurudi katika mpangilio bila kugombana na wafanyabiashara wadogo. Ameonyesha kuwa mji unaweza kusimamiwa kwa nidhamu bila chuki, na kwamba serikali inapokuwa thabiti, wananchi wanaelewa.

Mimi nampongeza kwa dhati Chalamila. Nashawishika kuwauliza wakuu wa mikoa mingine wako wapi? Inakuwaje miji yao imejaa wamachinga na hakuna hatua wanazochukua? Jiji kama Arusha, ukipita maeneo ya Stendi Sheikh Amri Abeid, barabara ya kwenda Unga Limited, hadi unashika tama. Mwanza waliondolewa Makoroboi kipindi fulani, ila sasa kila mtu anajua. Siwezi kutaja, ni kila kona ya nchi.

Naomba hapa nieleweke. Si kwamba nina roho mbaya nataka vijana hawa waondolewe wakose riziki, la hasha! Nalenga vijana hawa wakue. Wakue kiuchumi. Ilani ya CCM imetangaza kongani za viwanda kila wilaya. Nafahamu kuna wasomi wengi wanafanya kazi ya umachinga, wanaendesha bodaboda. Hizi kazi zinawapa fedha, lakini si kazi nyepesi kihivyo. Wamezizoea kwa kuwa hakuna mbadala.

Vijana hawa wakipata kazi za viwandani, ambazo watajiunga kwa ubia au mtu ataajiriwa afanye kazi kwa saa 8, alipwe mshahara mzuri, alipiwe bima ya afya, nyumba na awe na likizo, apate muda wa kuwasalimia ndugu na jamaa, hauwezi kumwona kwenye bodaboda. Vijana wengi wanapoteza maisha kupitia bodaboda kutokana na kufanya kazi hii karibu saa 24 na siku 7 kwa wiki. Wanalala kwenye vijiwe, mbu ni wao, mvua ni yao, baridi ni yao na kuporwa pikipiki ni kawaida.

Sitanii, vijana hawa wakipata kazi ya heshima, hauwezi kuwaona wakitembeza nguo. Uzuri vijana wa Tanzania wanaelewa. Kazi ikiwa inalipa bila manyanyaso wanaifanya kwa moyo mkunjufu. Nimeshuhudia nchi kama China kazi nyingi zinatokana na uwekezaji katika viwanda. Leo tunanunua urembo, hereni, vijiko, vikombe, glasi, visosi, nguo, mashati, T-shirt… kutoka China. Pamba inayozalishwa hapo nchini tukirejea wazo la Mwalimu Julius Nyerere ikatumika kuzalisha nyuzi, nyuzi zikazalisha vitambaa, vitambaa vikashonwa nguo, huo ni mnyororo wa ajira mrefu mno kuanzia shambani hadi kupata kitenge au shati.

Kuna wakati najiuliza, tunafeli wapi? Mwaka 2017 na 2018 niliandika makala nyingi za kilimo cha mihogo. Nikiri mwitikio wa Watanzania kulima mihogo, wakubwa kwa wadogo, ulikuwa mkubwa hadi nikaogopa. Tanzania ilikuwa ipate mkataba mnono nchini China wa kuuza mihogo, ila waziri akachelewesha kusaini mkataba wa afya ya mimea, wakaona ‘tunazingua’ wakahamishia mradi mkubwa Nigeria. Pamoja na kwamba Nigeria ni mbali kuliko Dar es Salaam au Bagamoyo kwenda China. Tujifunze kwa makosa ya aina hii, tusiyarudie.

Naamini eneo la kongani za viwanda kila wilaya nililolitaja hapo juu, halijapigiwa debe vya kutosha. Kuna kazi naimalizia, naomba kuahidi kuwa nitafanya kazi ya kujitolea sawa na wanaoanzisha makanisa au misikiti kuhubiri habari njema, mimi nitahubiri viwanda kwa ajira za vijana wetu. Uzoefu nilioupata kwenye kilimo cha mihogo, viwanda vikiongezewa mwendo, vijana wetu wanapata ajira.

Hapa si suala la ajira tu. Viwanda vikiwa vingi, tutapanua wigo wa kodi. Tutaondokana na hizi kodi za kuviziana, ambazo kila ukinunua umeme kupitia Luku serikali inakusanya Sh 1,500. Ukijichanganya ukawa na Luku 5, unalipa kodi ya kichwa Sh 6,000. Wamiliki wa maghorofa hao ndio wanaokomolewa. Kila ghorofa anatozwa Sh 7,500 kwa kila ghorofa kila mwezi.

Hii ni sera inayopalilia matumizi mabaya ya ardhi. Kuna watu wanajenga. Mwenye ghorofa kila mwaka anakamuliwa Sh 90,000. Nyumba ya kawaida analipishwa Sh 18,000. Hapa tunahamasisha watu wajenge nyumba za chini. Unakuta mtu anajenga vyumba 18, anatozwa Sh 1,500  kwa mwezi na yule ambaye ana vyumba vinne vya ghorofa anatozwa Sh 7,500. Haya yataondoka tukiwa na viwanda vya kutosha, tukauza nje ya nchi tukapata kodi za maana badala ya kukimbizana na wachuuzi.

Sitanii, lengo langu ni tuwaandalie maisha hawa vijana. Mwaka 2004 nilisafiri na Mzee Edward Ngoyai Lowassa (Mungu amlaze mahala pema peponi) kwenda Misri. Katikati ya Jiji la Cairo, tulikuta maghorofa ya wamachinga. Lowassa alivutiwa na mpango huo. Aliporejea akawasukuma Jiji wakajenga Machinga Complex. Wakubwa wakaanza dili. Wakaweka vizimba kama vya kufugia panya. Wakaruhusu watu wauzie chini. Jengo likasuswa, hadi leo sidhani kama lina faida.

Nasema tubadilike. Serikali itafute kama Sh bilioni 50. Maeneo kama Mbagala, Manzese na mengine mengi yenye msongamano wa wamachinga, serikali inunue majengo na kupandisha maghorofa kama National Housing ilivyofanya pale Karikoo eneo la Msimbazi kwenda Congo.

Haya yanawezekana, ila ni hadi tutakapoweka siasa kando. Leo tunampongeza Chalamila, wamachinga wakipiga kelele kidogo tu, walioshirikiana naye wananawa mikono wanasema ni lake!

Sasa namwambia kwa unyenyekevu, lakini kwa msisitizo: Operesheni hii isiishie mjini na Kariakoo pekee. Dar es Salaam ni mkoa mkubwa. Changamoto za wamachinga haziko mjini tu; ziko Mbagala, Temeke, Manzese, Sinza, Ubungo, Tabata, Kigamboni, Kimara, hata Gongolamboto… Kama tumeamua kurejesha mpangilio na hadhi ya jiji letu, basi tufanye kwa jiji lote, si sehemu ndogo tu. Leo eneo kama Banana, pale Hali ya Hewa ni kichekesho. Barabara nzuri imejengwa, kila jioni inamwagiwa mafuta ya wakaanga kuku, samaki, chipsi… Huu ni wakati wa kuonyesha kuwa mpangilio si wa eneo fulani, bali ni falsafa ya uongozi.

Sitanii, hatuwezi kuendesha operesheni ambayo mwisho wake ni kuwaacha wamachinga wakihangaika mitaani bila mwelekeo kama nilivyosema hapo juu.

Watu hawa wana familia, wana wajibu, na wana uhalali wa kufanya biashara kama Watanzania wengine. Ndiyo maana pendekezo langu ni kwamba serikali itenge Sh bilioni 50 mahsusi kwa ajili ya mpango mkubwa wa kununua maeneo mbalimbali jijini kama Manzese, Mbagala, pamoja na maeneo yaliyo karibu na vituo vikuu vya mabasi.

Fedha hizi zitumike kununua majengo ya zamani, maeneo yaliyotelekezwa, au hata viwanja ambavyo vinaweza kujengwa maghorofa ya kisasa kwa ajili ya wamachinga. Tujenge mabweni ya biashara yenye mpangilio: sakafu za kutosha, lifti, vyoo, usalama, sehemu za kuhifadhi mizigo, huduma za benki, kamera za usalama, sehemu za chakula na huduma za kijamii.

Tukifanya hivyo, tutakuwa tumewakwamua wamachinga kutoka kwenye biashara za kubahatisha hadi kwenye mazingira ya kisasa yanayoheshimu ubinadamu wao na thamani ya biashara zao.

Kwa kufanya hivyo pia, serikali itakuwa imeondoa tatizo la muda mrefu la kuwakimbiza wamachinga kutoka eneo moja hadi jingine bila suluhisho la kudumu.

Tutakuwa tumetatua tatizo milele, si kwa muda. Na zaidi ya hapo, jiji letu litapata sura mpya – sura ya mpangilio, ustaarabu na maendeleo.

Kwa mara nyingine, nasema hongera sana RC Chalamila kwa ujasiri na uwajibikaji. Endelea hivyo hivyo. Lakini sasa nasema: ongeza kasi, panua wigo, na hakikisha operesheni inafika hadi Mbagala, Manzese, Banana, Gongolamboto na maeneo yote ya Dar es Salaam. Nanyi Serikali Kuu mtieni moyo RC Chalamila. Tengeni fedha, jengeni  miundombinu, ili tuanzishe enzi mpya ya masoko ya maghorofa ya kisasa kwa wamachinga. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827