Na Theophilida Felician, JamhuriMedia, Pwani

Chama cha waganga wa tiba asili na tiba mbadala nchini TAMESOT kimeendelea kuwafikia waganga kikiwa na malengo mahususi ikiwemo ya kuwapa elimu ya kuwajengea uelewa na uwezo thabiti katika kutoa huduma ya tiba asili.

Hayo yanajiri mikoa kadhaa kutokana na katibu mkuu wa chama hicho Bw Lukas Joseph Mlipu kukutana na waganga na kuwapa dodoso lenye kuwaongezea ufahamu na ujuzi zaidi katika uboreshaji wa tiba asili.

Katibu mkuu Lukas akiwa mkoani Pwani kwa ziara ya kutoa elimu ameendelea kuwasisitiza mengi waganga ikiwemo ya kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya taaluma kama inavyoelekezwa na miongozo ya baraza la tiba asili na tiba mbadala pamoja na miongozo na kanuni za chama hicho ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Kiongozi huyo akiwa na waganga wa mkoa wa Pwani ameendelea kukemea matapeli wanaotumia jina la tiba asili kwa lengo la kujipatia fedha jambo ambalo limesababisha madhara ya ukatili mara kadhaa kwa wananchi.

Hata hivyo Katibu mkuu Lukas amewateua viongozi ngazi mbalimbali mkoa wa Pwani na viongozi wa wilaya za mkoa wa Morogoro kwalengo la kuendelea kukijenga chama kwa uongozi imara huku akitoa miongozo ya chama kwa wanachama na viongozi hao.

Ziara ya kiongozi huyo imehitimishwa mkoani Pwani na kuendelea mkoa wa Tanga.