Na mwandishi Wetu, Babati

MKOA wa Manyara umepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Sh327 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.

Katibu Tawala msaidizi sehemu ya mipango na uratibu, Lusungu Mwilongo ameeleza hayo mjini Babati kwenye kikao cha kamati ya ushauri (RCC) ya mkoa huo.

Mwilongo ameeleza kwamba bajeti hiyo imezingatia malengo mbalimbali ikiwemo maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, akifungua Bunge la 13, dira ya Taifa ya maendeleo 2050 na mpango wa nne wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.

Amesema katika mpango huo wa bajeti miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na halmashauri za wilaya itatekelezwa.

“Ni jukumu la viongozi na wananchi kuhakikisha kuwa wanashirikiana ili kutekeleza bajeti hii hasa hasa suala la kukamilisha kwa miradi ya maendeleo,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewataka viongozi na watumishi wa serikali kuhakikisha wanaacha alama katika utumishi wao wa kuitumikia jamii.

“Tusiache kumbukumbu ya vibao vya majina yetu tuu, hapana, tuhakikishe tunatumia nguvu kubwa na maarifa tuliyonayo katika kuwatumikia watu wetu wa Manyara na kuacha alama nzuri nyuma yetu,” amesema Sendiga.

Hata hivyo, amewapongeza wabunge wa mkoa wa Manyara, kwa namna wanavyowasemea wananchi wa eneo hilo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji, kilimo, mifugo na barabara.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Daniel Sillo ambaye pia ni mbunge wa Babati vijijini, amesema wananchi wana matarajio makubwa kwa viongozi wao katika kuwafikishia huduma za kijamii.

Sillo amesema kuanza mwezi Machi wabunge wa mkoa huo watakuwa Bungeni jijini Dodoma katika Bunge la bajeti hivyo wapiga kura wasipowaona wafahamu kuwa wanatekeleza wajibu wao wa kuwasemea.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa ya maendeleo kwa kuhudumia jamii ya wafugaji kwenye suala la maji, elimu na afya.

“Kwa sisi tulioishi maisha ya vijijini miaka hiyo tukiwa wadogo hatuna huduma za maji, au vituo vya afya au kutembea umbali mrefu kwenda shule, ndiyo ambao tunatambua kuwa serikali imefanya kazi,” amesema Ole Millya.