Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara

MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewataka wajasiriamali na wafanyabiashara kutumia fursa zinazotolewa na Serikali, ikiwemo kujitangaza (branding) bidhaa zao za kibunifu, ili kuongeza thamani na kuziwezesha kufika katika masoko ya kimataifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Utambuzi wa Bidhaa za Viwandani na Matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence), iliyofanyika juzi katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia – MUST, Kampasi ya Mtwara, Mkoani Mtwara, Mwaipaya alisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya bidhaa badala ya kuuza mazao ghafi.

“Serikali inasisitiza kutouza bidhaa ghafi bila kuziongezea thamani. Nawahimiza vikundi vya wajasiriamali vijana na kina mama waliojitokeza kupata mafunzo haya kuwa chachu ya kujiongezea kipato na kupanua biashara zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” alisema Mwaipaya.

Aidha, alieleza kuridhishwa kwake na hatua zinazochukuliwa na wajasiriamali katika kuongeza thamani ya mazao, hususan korosho, kupitia mnyororo wa thamani unaohusisha uzalishaji, uchakataji na uuzaji wa bidhaa zenye ubora unaokidhi masoko ya kimataifa.

Mwaipaya alibainisha kuwa mafunzo yaliyotolewa na Mbunifu wa Scan Code anayelelewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), na yaliyoratibiwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), yamelenga maeneo matatu muhimu.

Aliwahimiza wajasiriamali kuzingatia elimu hiyo, hususan katika suala la branding ili kujitofautisha sokoni.
Maeneo hayo matatu ni: Matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI).Matumizi ya Msimbo wa Papo (QR Code) na Uanzishwaji wa kanzidata ya wajasiriamali wa Wilaya ya Mtwara.

Alisisitiza kuwa teknolojia inakwenda kwa kasi kubwa, hivyo ni muhimu kwa wajasiriamali na wabunifu kuendana nayo, kwani AI imewezesha upatikanaji na usambazaji wa taarifa kwa haraka na kwa ufanisi.

Pia aliwahimiza wajasiriamali kutumia fursa ya mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 4 kwa vijana, kina mama na makundi maalum ili kukuza biashara zao.

Kwa upande wake, Meneja wa SIDO, Merina Mkuchu, alisema wanafurahia kuratibu semina hiyo kutokana na mwitikio mkubwa wa wadau, ikiwemo makundi ya wajasiriamali wanaolelewa na SIDO, uwepo wa COSTECH kama mlezi wa Kampuni ya Scan Code (L) Tanzania, pamoja na udhamini kutoka sekta binafsi uliowezesha mafunzo hayo.

Naye Afisa Uhusiano Mwandamizi wa COSTECH, Ndg. Faisal A. Jalil, alishukuru kwa mwaliko kutoka kwa SIDO na kueleza kufurahishwa na ubunifu wa bidhaa mbalimbali alizoziona, zikiwemo viungo, sabuni, korosho, siagi ya karanga (peanut butter) na pilipili.

Aliwasihi wabunifu kutosita kuomba ufadhili kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishwaji (Samia Innovation Fund), wenye masharti nafuu, ili waweze kuongeza thamani ya bidhaa zao, kujiongezea kipato, kupanua masoko ya kimataifa na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na kuongeza ajira kwa vijana.