Na Mwandishi Wetu, Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amewataka viongozi na watumishi wa serikali kuhakikisha wanaacha alama katika utumishi wao kwenye maeneo yao wanayoyaongoza.
RC Sendiga ameyasema hayo mjini Babati kwenye kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo kilichohusisha wakuu wa wilaya, wabunge, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri na vionjo mbalimbali.
“Tusiache kumbukumbu ya vibao vya majina yetu pekee katika maeneo tunayoongoza ila kazi zetu zibaki mioyoni mwa wale ambao tunawaongoza,” amesema RC Sendiga.
Pia, amewataka wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) na wakala wa barabara vijijini na mijini (TARURA) kwenye mkoa huo kukarabati barabara korofi kila wakati ili kuwezesha kupitika kwa urahisi katika kwa majira yote ya mwaka.

Amezitaka taasisi hizo zinazohusika na ujenzi wa barabara katika mkoa huo kuomba fedha za dharura za kukarabati barabara zinazoharibiwa hasa wakati huu mvua zinapoendelea kunyesha.
“Barabara ndiyo uchumi wa wananchi wa Manyara, kwani wanaweza kuondoka na kwenda sehemu moja hadi nyingine wakisafiri wao au bidhaa zao na mazao yao,” amesema RC Sendiga.
Ameeleza kwamba barabara nazo zinapaswa kukuwa na kuendelea ili nyingine zianzishwe upya kwani zinatoka ngazi ya udongo, changarawe, kokoto na kuwa za lami.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya ameeleza kuwa inapaswa ukanda mwingine wa Manyara, hasa Simanjiro na Kiteto napo pafunguke kwa barabara ya lami.
“Wabunge wote wa Manyara tunatakiwa tuwe na ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha tunafanikiwa kwa malengo ya kuhudumia watu wa eneo hili bila kuweka maslahi yetu binafsi ila ya wananchi,” ameeleza.
Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Lekaita ameshangazwa na kilomita 70 za ujenzi wa barabara ya lami ya Arusha – Simanjiro – Kiteto hadi Kongwa Dodoma, kuendelea kuzunguka jiji la Arusha badala ya barabara hiyo.

“Hizo kilomita 70 zingeanza pale kwa Mromboo Arusha zingefika Terrat wilayani Simanjiro na kusogeza barabara hiyo badala ya kilomita 15 zinazoishia kijiji cha Losinyai wilayani Simanjiro na haziendi kwenye uwanja mpya wa mpira ila zinapia sehemu nyingine,” amesema.
Meneja wa wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Manyara, Mhandisi Dutu Masele amesema katika eneo hilo, wanasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1,657.
Masele amesema kati ya barabara hizo kilomita 207 ni barabara kuu na kilomita 1,450 ni barabara za mkoa wa Manyara.
“Kilomita 207 za barabara kuu zote ni za lami na kilometa 52 za baraba za mkoa ni za lami na zilizobaki kilomita 1,398 ni za changarawe,” amesema Masele.
Amesema barabara zote kwa sasa zipo kwenye hali ya kuridhisha na zinapitika na wamejipanga kufanya matengenezo ya haraka sehemu zinazoathirika na mvua za masika.
Meneja wa wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) mkoa wa Manyara, Salim Bwaya amesema wanasimamia mtandao wa barabara za urefu wa kilomita 6,898.73.
Bwaya amesema kati ya barabara hizo kilomita 2,314.99 ni barabara unganishi na kilomita 3,348.64 ni barabara ujazio na kilomita 1,235.10 ni barabara jamii.
“Viwango vya barabara katika mtandao huu ni kilomita 41.162 za lami, kilomita 2,432.792 za changarawe na barabara za udongo kilomita 5,017.


