Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
KATIBU Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), James Sando, amesema mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha uwazi na ufanisi katika usimamizi wa rufaa za zabuni kwa kutumia mifumo ya kidijitali, hatua inayolenga kuongeza imani ya wadau katika mchakato wa ununuzi wa umma.
Sando alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na fursa za vijana kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Akizungumzia matumizi ya teknolojia, Sando alisema PPAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imekamilisha ujenzi wa Moduli ya Kupokea na Kushughulikia Malalamiko na Rufaa ndani ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).
“Moduli hii inatoa njia rahisi, ya haraka na yenye uwazi kwa wadau wote kushiriki katika mchakato wa usuluhishi wa migogoro ya ununuzi wa umma, hivyo kuimarisha imani katika mfumo huo,” alisema Sando.
Alifafanua kuwa tangu kuzinduliwa rasmi Februari 2025 na Wizara ya Fedha, jumla ya malalamiko 549 (Administrative Reviews) yamewasilishwa na kushughulikiwa na taasisi nunuzi kupitia moduli hiyo. Aidha, rufaa 26 zimewasilishwa na kushughulikiwa na PPAA kwa njia ya kielektroniki.
Kwa mujibu wa Sando, katika kipindi cha uongozi wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka hiyo imesajili mashauri takriban 196 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya ununuzi wa umma.

Alisema katika baadhi ya mashauri hayo, Mamlaka ya Rufani ilizuia utoaji wa tuzo za zabuni 43 zenye thamani ya Shilingi bilioni 586.502 kwa wazabuni waliokosa uwezo wa kifedha na sifa za kitaalamu zinazohitajika kutekeleza zabuni husika.
“Hatua hii imezuia utekelezaji usioridhisha wa miradi ambayo ungesababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo endelevu kwa wananchi,” alisema Sando.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaamini kuwa usuluhishi wa migogoro hauwezi kufanikishwa katika mazingira ya ubaguzi au pale haki za kiuchumi na kiraia hazitolewi kwa usawa.
“Uamuzi wa kuzuia utoaji wa tuzo kwa wazabuni 43 waliokosa sifa unaimarisha mchakato wa usuluhishi wa migogoro, ambao ni miongoni mwa falsafa nne (4Rs) za Mheshimiwa Rais,” alisisitiza.
Kuhusu maboresho ya kisheria, Sando alisema mwaka 2023 Serikali ilitunga upya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, ikifuatiwa na Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 pamoja na Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2025.
Alieleza kuwa maboresho hayo yameleta ufanisi katika sekta ya ununuzi na ugavi kwa kuimarisha dhana ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi na kwamba sheria mpya imepunguza muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa katika hatua mbalimbali.

Kwa mujibu wake, muda wa kuwasilisha malalamiko kwa taasisi nunuzi umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi tano, huku muda wa Afisa Masuuli kushughulikia malalamiko ukipunguzwa kutoka siku saba hadi tano za kazi.
Aidha alisema, muda wa kuwasilisha rufaa PPAA umepunguzwa kutoka siku saba hadi tano za kazi, na muda wa mamlaka hiyo kushughulikia rufaa umepunguzwa kutoka siku 45 hadi siku 40.
Sando aliongeza kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na taasisi nyingine za usimamizi wa ununuzi wa umma, PPAA iliandaa Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2025 zilizotangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali Januari 31, 2025 kupitia GN Na. 65/2025.
Alisema moja ya maboresho muhimu ni sharti la kuwasilisha malalamiko na rufaa kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).
Sando alisema takwimu hizo zinaonesha mafanikio ya awali ya matumizi ya moduli hiyo katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika mchakato wa ununuzi wa umma nchini.


