Na Mwandishi Maalum,Ruvuma
MAKAMU wa Rais Dkt Emanuel Nchimbi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwa kilele cha kumbukizi ya miaka 120 ya mashujaa wa vita ya Majimaji itakayofanyika tarehe 27 Februari mwaka huu katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Akizungumza na Waandishi wa habari Ikulu ndogo mjini Singea,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas alisema,Makamu wa Rais atawasili kesho Alhamis tarehe 26 majira ya saa tisa alasiri katika kiwanja cha ndege cha Songea na atapokelewa na viongozi wa Chama na Serikali
Abbas alisema, tarehe 27 atatembelea kwenye mnara wa kumbukumbu eneo walillonyongwa mashujaa wa vita ya maji maji eneo kuzindua jengo la wazee wa baraza la mira na desturi lililopo eneo la Songea klabu.
Kwa mujibu wa Abbas,baada ya hapo atatembelea eneo la makumbusho na ataweka upinde na ngao kwenye mnara wa mashujaa na kuongea na wananchi waliohudhuria kumbukizi hizo.
“Natumia nafasi hii kuongea na waandishi wa habari,nawaomba muwahabarishe wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, wajitokeze kwa wingi kuanzia kwenye mapokezi hapo kesho katika kiwanja cha ndege Songea na tarehe 27 kwenye viwanja vya mashujaa ambako kutakuwa na kilele cha maadhimisho hayo”alisema Abbas.
Alisema,maadhimisho ya kumbukizi ya mashujaa wa vita vya majimaji yalitanguliwa na shughuli mbalimbali katika wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma kuanzia tarehe 19 Februari ambapo kulikuwa na matamasha ya kumbukizi na utamaduni na uzinduzi rasmi wa mahadhimisho ya mwaka huu yalifanyika tarehe 23 mwezi huu.


