Na Jeston Kihwelo, WANMM, JamhuriMedia, Mbeya
Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mbeya Siyabumi Mwaipopo amewataka wawekezaji wote ambao hawajaendeleza maeneo yao au wameyatelekeza kujitokeza mara moja katika Ofisi yake kwa ajili ya kupatiwa utaratibu wa kisheria, ikiwemo kulipia malimbikizo ya madeni wanayodaiwa na Serikali.
Amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wamiliki watakaokaidi maelekezo hayo.
“Wawekezaji wote wanapaswa kuzingatia masharti ya umiliki na kuendeleza maeneo yao kwa mujibu wa sheria. Watakaoshindwa kufanya hivyo Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao ikiwemo kurejesha maeneo hayo serikalini ili yatolewe kwa wawekezaji wengine wenye nia na uwezo wa kuyaendeleza,” ameeleza.
Aidha, amewaomba wawekezaji kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Jiji la Mbeya kwani kutokana na ukaguzi huo, maeneo mengi ya uwekezaji yako wazi.
Kwa upande wake Kiongozi wa Wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jacob Ngowi, amesema kuwa tathmini ya awali imebaini kuwa mapaka kufikia Februari 25, mwaka huu, jumla ya maeneo 127 yamebainika kuwa katika hali ya kutoendelezwa.
Amesema katika ukauguzi huo imegundulika kuwa, baadhi ya maeneo yamebadilishwa matumizi bila kibali, mengine yamekiuka masharti ya umiliki, huku viwanda kadhaa vikibaki katika hali ya magofu.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea na zoezi ya ukaguzi wa maeneo yote nchini ambavyo hayajaendelezwa au wamiliki wamevunja masharti ya umiliki ikiwemo ulipaji wa Kodi ya Pango la Ardhi, maeneo ambayo wawekezaji wamekiuka masharti ya uwekezaji ili kuyabaini na kuhakikisha ardhi inatumika kwa tija, kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Mbeya ikiwemo kutoa ajira kwa vijana kwa kupitia uwekezaji kwa njia ya viwanda.






