Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mirerani

CHANGAMOTO ya kutokamilika kwa daraja la barabara ya Mirerani – Mbuguni eneo la mkuyuni mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, limepatiwa ufumbuzi baada ya mafundi kulikamilisha.

Wakati huu ambapo mvua zinaponyesha imekuwa faraja kwa wakazi wa eneo hilo wanaopita katika barabara hiyo inayounganisha mikoa ya Manyara na Arusha.

Msimamizi wa ujenzi huo kutoka wakala wa barabara nchini TANROADS mkoa wa Manyara, Aminiel Lyimo amesema daraja hilo limekamilika.

Lyimo amesema wamemaliza kulifunika na zege na sasa inasubiriwa likauke ili lianze tena kutumika na magari yaanze kupita kama awali.

“Sasa hivi tupo kwenye umwagiliaji na kusubiri siku 28 za kukauka ili magari yaanze kupita katika daraja hilo,” amesema Lyimo.

Amesema hivi sasa wameandaa njia ya mchepuko yenye daraja la muda kwa ajili ya vyombo vya usafiri na watu kupita wakisubiri likauke wapite.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Raphael Ombade amesema hali hiyo inawapa matumaini kwani ameshuhudia daraja hilo kukamilika na kusubiri likauke na watu kuanza kupita.

“Hii ya kuweka njia mchepuko na daraja la muda itasaidia watu na magari kupita wakati huu tukisubiria kukauka kwa daraja hilo,” amesema Ombade.

Mkazi mwingine wa eneo hilo John Sarakikiya amewapongeza TANROADS kwa kukamilisha daraja hilo kwani barabara hiyo inategemewa kusafiria na kufika jijini Arusha kwa ufupi.

“Tunaishukuru serikali kwani awali yule mkandarasi aliyepewa dhamana ya kujenga daraja la barabara hii alifanya uzembe na kuchelewesha kujenga ila sasa TANROADS wameingilia kati na kukamilisha,” amesema Sarakikiya.

Amesema wakati huu ambapo mvua zinaponyesha itakuwa vyema kwa daraja hilo kukamilika na likikauka lianze kutumika kama ilivyokuwa awali.