Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imetoa tuzo maalumu kwa wadau zaidi ya 10 ambao wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na halmashauri hiyo ikiwemo kuchangia shughuli za kitaifa.
Akikabidhi tuzo hizo jana kwenye kikao cha madiwani Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Ghullam Hussein Remtullah amempongeza Mkurugenzi Mtendaji Dkt John Pima kwa kuandaa tuzo hizo.
Ameeleza kuwa tuzo hizo ni muhimu sana kwa kuwa zinadumisha ushirikiano na mahusiano mazuri na wananchi wanaojitolea kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo matukio makubwa ya kitaifa yanayofanyika katika manispaa hiyo.
‘Hawa tunaowapa tuzo leo ni wakulima, wafanyabiashara na wafugaji ambao wamekuwa wakijitolea kwa hali na mali kuishika mkono halmashauri ili kufanikisha mambo mbalimbali, walitoa chakula, fedha na mifugo’, amesema.
Mstahiki Meya amebainisha kuwa manispaa inatambua na kuthamini mchango wao ndiyo maana leo wamekabidhiwa tuzo hizo, aliwaomba kuendelea na moyo huo kwa kuwa manispaa pekee yake haiweze kufanikisha kila kitu pasipo wadau.
Aidha Mstahiki Meya amegawa vishikwambi kwa Watendaji wa Kata zote 29 za manispaa hiyo ili kuwarahisishia utendaji wao hususani katika suala la usajili wa makazi ya wananchi, biashara na utoaji taarifa zinazohusu Kata zao.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Neema Kapesa amemweleza Mstahiki Meya, Mkuu wa Wilaya na Madiwani kuwa zoezi la utoaji tuzo kwa wadau wa maendeleo litakuwa endelevu ili na wadau wengine wahamasike.
Kuhusu vishikwambi, amedokeza kuwa vitasaidisa kuboresha zoezi la usajili wa makazi ya wananchi katika Kata zao ikiwemo biashara na shughuli nyingine zinazofanyika katika maeneo hayo.







