Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange ametoa wito kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuzungumzia faida za Muungano na umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa wananchi wanaowangoza.

Ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali alipowasili katika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kuanza ziara ya kukagua shughuli za mazingira katika Wilaya ya Karagwe, leo Februari 25, 2026.

Dkt. Dugange amesema kuwa kila kiongozi kwa nafasi yake pamoja na kuzungumia masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi, ni muhimu akatumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania namna Muungano ulivyo na faida.

Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinashirikiana katika kuzipatia ufumbuzi hoja za Muungano na hivyo kuendelea kujenga imani kwa wananchi wake.

Alisema kulikuwa na hoja za Muungano 25 na tayari hoja 22 zimeshapatiwa ufumbuzi na kusalia hoja tatu ambazo Serikali inaendelea kuzitafutia ufumbuzi kupitia vikao vya ushirikiano wa pande zote mbili za Muungano.

“Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri agenda za Muungano na Mazingira ziwe za kudumu, mna nafasi ya kuzungumzia faida za Muungano,” alisisitiza Dkt. Dugange.

Kwa upande mwingine, alisisitiza umuhimu wa viongozi hao na wananchi kwa ujumla kushiriki katika shughuli mbalimbali za hifadhi ya mazingira ambayo ndio agenda ya dunia.

Naibu Waziri huyo alifafanua kuwa athari za mazingira zikiwemo mabadiliko ya tabianchi hazitabiriki na kwamba husababisha mvua nyingi kuliko kawaida, ukame, vimbunga na ukame huleta changamoto za kiafya.

Dkt. Dugange Alisema kuwa dhamira ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Ris ni kuhakikisha nchi inakuwa salama kwa kukabiliana na changamoto za kimazingira na ndio maana inatekeleza miradi mbalimbali kuwasaidia wananchi.

Halikadhalika, alisema kuwa kutokana na umuhimu huo, mojawapo ya nguzo tatu zilizopo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inazungumzia hifadhi ya mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Yahya Kido alipongeza juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa juhudi zake katika kuhakikisha hifadhi ya mazingira inakuwa endelevu.