Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa rai kwa viongozi kuwa wabunifu ili kuendana na kasi ya uchumi wa dunia kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na mifugo, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

Kunenge aliyasema hayo Februari 25, 2026 katika Mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Pwani uliowakutanisha Meya wa Manispaa, wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi na madiwani.

Alisema ni muhimu kwa kila kiongozi kujitathmini namna anavyochangia kuleta mabadiliko chanya katika eneo lake kwa lengo la kuwapatia wananchi maendeleo endelevu.

“Wajibu wetu ni kwenda sambamba na kasi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kilicho cha umuhimu ni alama tunayoiacha kwa wananchi kwa kuleta maendeleo ya haraka, kwani dunia ya leo ni ya ushindani, hivyo tunapaswa kufanya kazi kwa umoja,” alisisitiza Kunenge.

Aidha, amewataka viongozi kuweka mkazo katika kuvutia na kusimamia uwekezaji kwenye maeneo yao, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato ya halmashauri na kuuchochea mkoa kupiga hatua zaidi kiuchumi.

Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Pwani, Mohamedi Usinga, aliwahimiza viongozi kuwa mfano wa kuigwa kwa kusimamia miradi ya maendeleo na kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.

Katika mkutano huo, viongozi wapya wa ALAT Mkoa wa Pwani walichaguliwa ambapo nafasi ya Mwenyekiti ilichukuliwa na Mohamed Usinga, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, nafasi ya Makamu Mwenyekiti Gulam Mohammed, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia.

Jumuiya ya Wanawake wa Serikali za Mitaa (WASEMI) Badria Shaha, Diwani wa Viti Maalum kutoka Kisarawe, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti na Shumina Rashidi Diwani kutoka Bagamoyo, kuchukua nafasi ya Katibu.