Na Mwandshi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tume ya Ushindani (FCC) imeanza kutumia Mfumo wa Ukaguzi wa Bidhaa wa Pamoja (TANOGA) unaofanya kazi kwa ushirikiano na mamlaka nyingine za serikali.

Akizungumza hivi karibuni katika semina ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari iliyofanyika Februari 23, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Uthibiti wa Bidhaa Bandia wa FCC, Salvator Chuwa, lengo la kuingia katika mfumo huo ni kudhibiti bidhaa bandia.

Kwa mujibu wa Chuwa, lengo jingine la mfumo huo ni kurahisisha shughuli za ukaguzi wa bidhaa na kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira rafiki ya biashara, huku wamiliki wa nembo za bidhaa nao wakipata thamani halisi ya uwekezaji wao.

Ametaja lengo jingine kuwa ni kuwalinda walaji wapate thamani halisi ya bidhaa wanazotumia na zenye kukidhi matarajio yao.

“Hatuna muda mrefu sana tangu tumeingia katika mfumo huo. Utekelezaji wetu unategemea mfumo wa kidijitali unaotambua mizigo yenye vihatarishi kwa kutumia TANOGA. Kupitia mfumo huo, sasa kibali cha forodha kitatolewa baada ya ukaguzi na idhini ya FCC,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema FCC imeanzisha Daftari la Kielektroniki la Alama za Biashara linalowezesha wakaguzi kuthibitisha papo kwa papo uhalali wa alama za biashara, nchi iliyotengeneza bidhaa na wazalishaji walioidhinishwa kabla ya kuruhusiwa kuingia sokoni.

Amesema bidhaa zenye shaka huzuiliwa mara moja na notisi za ukamataji kutolewa na wahusika wanakabiliwa na adhabu ikiwamo faini, kutaifisha na kuharibu bidhaa bandia.

Amesema wamiliki wa alama za biashara wanatakiwa kuwasilisha maombi FCC yakiambatanisha nyaraka husika na mkaguzi mkuu atazipitia ndani ya siku 21 kabla ya kuidhinisha au kukataa na zilizoidhinishwa huingizwa katika daftari rasmi.

Ametaja changamoto zinazojitokeza kuwa ni uelewa mdogo kwa baadhi ya waagizaji na wafanyabiashara wadogo kuhusu mchakato wa kurekodi alama za biashara, utegemezi wa mifumo ya kidijitali na uwezekano wa wafanyabiashara haramu kutumia njia zisizo rasmi za mipakani.

“Daftari hilo lina faida kubwa kwa sababu linalinda usalama wa watumiaji, linaimarisha ushindani wa haki kwa biashara halali, linaongeza mapato ya serikali kwa kupunguza ukwepaji kodi na unaongeza imani kwa wawekezaji,” amesema.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema wamefanya marekebisho ya sheria kwa ajili ya kufikia dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza biashara hapa nchini na kulinda walaji dhidi ya bidhaa zisizo na ubora.

“Tumefanya marekebisho ya sheria kama alivyosema Rais Samia kwamba tufungue milango kwa wawekezaji na kukuza biashara,” amesema.

Pia amesema marekebisho hayo yanalenga kudhibiti bidhaa bandia, kupambana na matangazo ya upotoshaji na kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia misingi ya ushindani wa haki.

Amesema kuenea kwa bidhaa bandia kunahatarisha afya za wananchi, kunapunguza mapato ya serikali na kuwakosesha wafanyabiashara halali fursa ya kufanya na kukuza biashara zao.