Na Deodatus Balile, Nairobi

Kifo cha Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kimeacha simanzi nchini, lakini pia kimeacha funzo na ujumbe mzito kwa taifa letu.

Tangu kutokea kwa kifo chake tumeshuhudia jambo ambalo kwa muda mrefu halijawahi kutokea – Watanzania kuungana, si kwa majukwaa ya siasa au kampeni, bali kwa moyo mmoja wa maombolezo, heshima na mshikamano. Kifo chake kimeonyesha kuwa bado tuna nguvu ya kuungana kama familia moja kitaifa.

Sitanii, mazingira ya ibada ya mazishi katika Kanisa Kuu la St. Joseph yameacha taswira mpya kwa nchi yetu. Ni kwa muda mrefu hatujawa na tukio la kijamii linalokutanisha viongozi wakuu watatu; Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika tukio moja na kwa wakati mmoja la kijamii.

Wiki iliyopita pale St. Joseph tumeona Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk. Balozi Emmanuel Nchimbi na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba wakiwa chini ya dari moja la Kanisa Kuu la Mt. Joseph. Si hilo tu, viongozi wa kidini, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Dk. Abubakar Zubeiry.

Haikuishia kwa viongozi wa dini tu, viongozi wa vyama ya siasa kuazia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee Stephen Wassira, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, aliyekuwa mgombea wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina na wengine wengi walikuwapo.

Sitanii, amani ilitamalaki kanisani. Hakukuwapo mashine ya kukaguana kabla ya kuingia kanisani, sawa na ilivyokuwa

Pugu alikozikwa Kardinali Pengo. Matukio yote hayo yaliyohudhuriwa kwa uzito unaostahili, hayakuwa na mbwa wala mashine za kukaguana na yamefanyika kwa amani.

Serikali ilikuwa imesimama kama kitu kimoja – mawaziri, viongozi waandamizi na watumishi wa umma walijitokeza kwa wingi kutoa heshima za mwisho. Lakini pia kulikuwa na jambo jingine kubwa zaidi: viongozi wa vyama vya siasa, ambao kwa miaka ya karibuni wamekuwa wakionekana kutofautiana na kugawanyika, walikaa pamoja, wakasali pamoja na kuomboleza pamoja. Jambo hili halikuwa la kawaida, na halitakiwi kupita hivi hivi bila kutafakari.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikizungumza juu ya maridhiano, majadiliano na haja ya kutengeneza taifa lenye umoja wa kweli. Mara nyingi mijadala ya aina hii imekwama kutokana na mihemko, misimamo ya kisiasa na historia ya kutokuvumiliana. Lakini kifo cha Kardinali Pengo kimetupa somo rahisi: kuna jambo kubwa kuliko siasa – utu, ubinadamu na mustakabali wa Tanzania.

Katika tukio hili tumeshuhudia kuta zilizojengwa na tofauti za kisiasa zikibomoka. Tumeshuhudia wakipeana mikono badala ya kupishana, macho yakiongea lugha moja badala ya kutiliana shaka, na mioyo ikikutana katika maombolezo badala ya ushindani. Huu ni ushahidi kwamba Watanzania tunaweza kukaa pamoja, tunaweza kusikilizana na tunaweza kuamua kusonga mbele kama taifa moja – iwapo tu tutajipa nafasi.

Ndiyo maana napendekeza kama taifa tuitumie fursa hii adhimu. Kifo cha Kardinali Pengo kimetupa mazingira sahihi ya kuanzisha mazungumzo mapya kati ya vyama vya siasa, serikali na wadau wengine muhimu. Tusisubiri tukio jingine la majonzi kutukutanisha.

Tuanzishe meza ya mazungumzo sasa – mazungumzo yenye lengo moja tu, kujenga Tanzania yenye umoja, haki na maridhiano ya kudumu.

Sitanii, kifo cha Kardinali Pengo kimetuonyesha njia. Kimetufundisha kuwa tofauti zetu si kikwazo, bali ni rasilimali zinazoweza kutufanya kuwa taifa lenye nguvu zaidi. Kimetukumbusha kuwa uhasama hauna faida, na kwamba maridhiano ni mtaji wa maendeleo. Leo vyama vya siasa vimekutana, serikali imejumuika na wananchi kutoka makundi mbalimbali walioungana kwa sauti moja kuomboleza. Tusiiache roho hii ipotee.

Kama taifa, tunao wajibu wa kuenzi urithi alioacha Kardinali Pengo – urithi wa mazungumzo, kuwa wakweli, uvumilivu, uungwana na upendo wa taifa. Huu ndio wakati wa kuandika ukurasa mpya. Tukiutumia vema, historia itakumbuka kwamba kifo chake hakikuwa mwisho, bali mwanzo wa Tanzania mpya, iliyojaa umoja na mshikamano.

Sitanii, mimi nimepata fursa ya kumfahamu Kardinali Pengo angalau kwa miaka zaidi ya 25. Nilihojiana naye na siku naandika kitabu cha Historia ya Parokia ya Roho Mtakatifu Kitunda, aliniwekea saini yake katika neno la utangulizi la kitabu hiki. Nilimfuata nyumbani kwake Kurasini akaniwekea saini.

Kardinali Pengo alikuwa na mawazo huru. Najua baadhi hamkumbuki. Mwaka 2010 kuelekea Uchaguzi Mkuu alitoa kauli ngumu mbili vijana walipokuwa wanaandamana. Alisema: “Vijana hawa wanarusha mawe, kwa sababu hawana risasi.” Hii ilikuwa kauli nzito kweli. Imejaa falsafa ndani yake, lakini pia uhalisia wa wazi. Tumeshuhudia yaliyotokea Oktoba 29, 2026. Hapa, tusiruhusu yaliyotokea wakati huo yakatokea tena. Madhara yamekuwa makubwa.

Hakuishia hapo. Kwa nia ya kuwataka CCM wajisahihishe, nadhanii aliona kama hawamsikilizi. Alitoa kauli nyingine ngumu ambayo siirudii, kwa wanaokumbuka ilihusisha neno “kichaka cha…” Naishia hapo. Baada ya kauli hiyo, CCM wakaanzisha operesheni vua gamba.

Mwaka 2018, Kardinali Pengo alitofautiana hadharani na maaskofu wenzake, walipotoa waraka alioona unaikandamiza CCM katika mazingira aliyoona yalikuwa ya uonevu kwa chama hicho. Baada ya kauli hiyo, Askofu Josephat Gwajima ndipo akaja na kauli ya “…amekula maharage ya wapi?” Matusi aliyoongeza dhidi ya Kardinali Pengo siyaandiki.

 Sitanii, binafsi napenda mtu ambaye anaweza kumsema mtu au taasisi au chama kwa makosa yake, lakini akaitetea taasisi au chama au mtu akiona anaonewa. Huyo ndiye aliyekuwa Kardinali Pengo. Niseme kwangu mimi nimejifunza hili kutoka kwake.

Leo mtu akikosea namwambia hapohapo na yanaisha, nikiona anaonewa nitamtetea hapo hapo bila kujali kuwa niliwahi kumkosoa. Naamini katika msimamo wa aina hiyo, badala ya kushikilia kinachoitwa msimamo ‘usiyoyumba’, hizo ni harakati.

Kusimamia ukweli, ndilo tumaini analotuachia Kardinali Pengo –  tumaini la taifa linaloweza kuungana tena. Tuitumie fursa na mafundisho tuliyopata kwenye kusanyiko hili, itusaidie kama taifa tuanze safari ya maridhiano aliyoianzisha Rais Samia Suluhu Hassan. Wenye kesi zifutwe, ila nao wakirejea uraiani washiriki kujenga taifa badala ya kulibomoa. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827