Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametoa hotuba muhimu jana Jumatatu kuhusu sera ya silaha za nyuklia za nchi hiyo katika wakati washirika wake wa Ulaya wana wasiwasi juu ya vitisho vinavyoongezeka kutoka Urusi.

Katika hotuba hiyo, Rais Macron amesema Ufaransa itaongeza idadi ya silaha zake za nyuklia na kufanya mageuzi makubwa ya kisera ya namna ya kuzitumia kama kinga dhidi ya uhasama kutoka nje.

Mabadiliko hayo yatahusisha Ufaransa kuruhusu kwa mara kwanza kupelekwa kwa ndege za kivita zenye makombora yake ya nyuklia kwa washirika wake kadhaa wa Ulaya.

Ufaransa ndiyo taifa pekee ndani ya Umoja wa Ulaya lenye hazina ya silaha za nyuklia na kwa miaka yote sera yake imekuwa ni kuzitumia kama kinga ya kulinda maslahi yake.