Israel imeendelea kuyashambulia maeneo kadhaa ndani ya Iran usiku wa kuamkia leo na Iran nayo imejibu kwa kuvurumisha makombora ya masafa kuelekea Israel na kwenye nchi kadhaa za ghuba ya Uajemi.
Mitikisiko mikubwa ilisikika kwenye mji mkuu wa Iran, Tehran, huku jeshi la Israel likisema limeishambulia pia miji mingine na kukilenga kwa mabomu kituo kimoja cha nyuklia.
Picha za Satelaiti zimeonesha paa la jengo la ikulu ya rais mjini Tehran limeharibiwa, ingawa Iran haijatoa taarifa yoyote kuhusu shambulizi hilo. Makombora ya Iran yaliulenga mji wa Tel Aviv na Israel imeripoti raia wake kadhaa wamejeruhiwa kutokana vishindo vya makombora.
Katika hatua nyingine, jeshi la Marekani limesema tangu kuanza kwa vita limeyashambulia zaidi ya maeneo 2,000 ndani ya Iran ikiwa ni pamoja na meli za kivita na mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran.



