Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu (AfCHPR) na Watu imetaka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua hatua za kikatiba na kisheria kurekebisha kifungu cha Katiba kinachozuia kupingwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais mahakamani.

Mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha ilitoa uamuzi huo leo Machi 6, 2026 katika shauri la Ado Shaibu na Wengine dhidi ya Tanzania, baada ya kubaini kuwa kifungu hicho kinakiuka baadhi ya haki za msingi za binadamu.

Shauri hilo lilifunguliwa na raia sita wa Tanzania ambao ni Ado Shaibu, Ezekiah Dibogo Wenje, Omar Musa Makame, Dorah Seronga Wangwe, Enock Weges Suguta na Kassim Ali Haji, wote wakiwa wanachama wa chama cha siasa cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo).

Waombaji hao waliiomba Mahakama ichunguze madai yao kwamba haki zao za kiraia na kisiasa zilikiukwa kabla, wakati na mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 nchini Tanzania.

Katika hatua ya awali, Tanzania iliipinga Mahakama hiyo ikidai kuwa haina mamlaka ya kushughulikia masuala yanayohusu mamlaka ya mahakama za ndani ya nchi, hata hivyo mahakama ilitupilia mbali hoja hiyo na kueleza kuwa ina mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayohusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu zinazolindwa na mikataba ya kimataifa ambayo nchi husika imeridhia.

Mahakama pia ilieleza kuwa Tanzania iliwasilisha tamko la kuruhusu watu binafsi kufungua mashauri dhidi yake mwaka 2010 chini ya Itifaki ya Mahakama hiyo, hivyo iliridhika kuwa ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo licha ya nchi hiyo kuliondoa tamko hilo mwaka 2019.

Katika uchambuzi wake wa kukubalika kwa shauri hilo, Tanzania iliwasilisha mapingamizi matatu, ikiwamo madai kuwa maombi hayo yalitegemea taarifa za vyombo vya habari pekee.

Mahakama ilibaini kuwa pamoja na taarifa hizo, kulikuwa pia na ushahidi mwingine kama hati za kiapo, hivyo ikatupilia mbali pingamizi hilo.

Mahakama ilikubaliana na Tanzania kuwa baadhi ya madai ya waombaji hayakuwa yametumia kwanza njia zote za kisheria ndani ya nchi. Hata hivyo, iliruhusu kusikilizwa kwa hoja kuhusu kukosekana kwa utaratibu wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais katika mahakama za ndani.

Katika uamuzi wake kuhusu hoja za msingi, Mahakama ilibaini kuwa kifungu cha Ibara ya 41(7) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, kinachozuia mahakama kuchunguza au kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais baada ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi, kinakiuka haki ya kupata haki na usikilizwaji wa haki kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

Kutokana na uamuzi huo, Mahakama imeiamuru Tanzania kuchukua hatua zote muhimu za kikatiba na kisheria ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ili kurekebisha kifungu hicho cha Katiba na kukifanya kiendane na masharti ya mkataba wa haki za binadamu.

Mahakama pia imeelekeza kuwa kila upande katika shauri hilo utagharamia gharama zake wenyewe.