Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Chama kitaendelea kusimama imara kuwaletea maendeleo Watanzania kwa kuwa ndilo jukumu lake la msingi.

Aidha, amewataka wana CCM kutambua kuwa uchaguzi una gharama na moja ya gharama zake ni hasira hususani kwa walioshindwa, hivyo wasikubali hasira iwapeleke katika hasara.

Wasira ameyasema hayo leo Machi 26, 2026 alipozungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ofisi za Chama Mkoa wa Geita ambalo ujenzi wake unatarajiwa kutumia sh bilioni 1.5.

“Chama chetu madhumuni yake ni mengi lakini kubwa ni kukamata dola, lakini watu wanatuuliza nyinyi mnataka kukamata dola ya nini, ukisoma katiba yetu nendeni mkasome madhumuni ni pamoja na kukamata dola, madhumuni makubwa kuliko yote ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, hiyo ndiyo kazi kubwa ya chama chetu.

“Sasa mnataka maendeleo ya Mkoa wa Geita lakini nyinyi ofisi yenu ya wasimamizi wa maendeleo mmejibanza kwenye vibanda, mnaweza kuulizwa maendeleo gani hayo yanayoweza kuletwa na chama hakina hata anuani.

“Kwa hiyo uko uhusiano kati ya jengo hili na wajibu wetu wa kusimamia maendeleo na tunasimamia maendeleo ndio maana tunataka dola, maana dola inatoza kodi tunajenga zahanati, dola inatoza kodi tunajenga chuo, dola inatoza kodi tunajenga miradi mingi ya maendeleo,” alisema.
Wasira alisema mtu yeyote ambaye anasema hakuna maendeleo yaliyofanyika huenda ana matatizo binafsi kwa kuwa kazi kubwa yenye kuonekana imefanyika.

“Hatumtukani lakini na yeye naye tunadhani ana matatizo ya kufikiri kwa sababu vitu tunavyofanya vinaonekana.

“Nimetoka Mwanza saa nne nimefika Geita saa tano kwa daraja lile la Magufuli kama lisingekuwepo ningefika hapa saa saba maana ningesubiri feri (kivuko) lakini tunafanya na hayo tunayoyafanya ndiyo ynayoeleza ukuu wa CCM katika kutekeleza majukumu yake ya kusaidia maendeleo ya watu na viongozi wetu wanachaguliwa na watu wenyewe,” alisema Wasira akitoa mfano wa sehemu ya maendeleo yaliyofanyika.ASISITIZA UVUMILIVU

Mbali na hilo, Wasira alisema kunapofanyika uchaguzi ni muhimu kuvumilia hususan kwa wale ambao wamekosa nafasi ya kufikia malengo yao ya kisiasa.

“Ninataka niwaombe wanachama waliopo hapa wajitahidi sana kuwa na kifua kipana maana uchaguzi una gharama na ghamarama yake nyingine ni hasira tu, ukishindwa unakasirika sana, hiyo nayo ni hasara, unaweza ukakasirika lakini ukasirike kidogo tu maana ukikasirika sana presha ikipanda unaweza ukaugua halafu hasira ikageuka kuwa hasara.

“Kwa hiyo mambo ya uchaguzi haya yakipita tuwe tunakubali kwamba yamepipita yalivyopita sasa turudi pamoja tujenge chama chetu tujiimarishe,” aliwaeleza.