Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Vangimembe Lukuvi, umeagwa leo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, huku viongozi na wananchi wakimwelezea kama nguzo muhimu ya uongozi wa Taifa.

Akizungumza leo Machi 27,2026 kwenye shughuli hiyo Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba amesema taifa limepoteza kiongozi mahiri na mwaminifu aliyekuwa na mchango mkubwa katika kusimamia na kuratibu shughuli za Serikali kwa ufanisi mkubwa.

Amesema Lukuvi alikuwa kiongozi mkomavu wa kisiasa mwenye ushawishi mkubwa, aliyesimamia majukumu yake kwa weledi na kujitolea, hali iliyomfanya kuaminiwa katika vipindi mbalimbali vya uongozi wa Serikali.

Dk. Nchemba ameeleza kuwa marehemu alikuwa mlezi na mshauri wa viongozi wengi, wakiwemo wabunge na mawaziri, ambapo mara nyingi alitoa mwelekeo sahihi kwa utulivu na hekima pale changamoto zilipojitokeza.

Ameongeza kuwa Lukuvi alikuwa na uwezo wa kipekee wa kueleza masuala magumu kwa lugha rahisi, jambo lililosaidia kuongeza ufanisi wa utendaji ndani ya Serikali na taasisi zake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametumia jukwaa hilo kuwataka Watanzania kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu, akionya dhidi ya upotoshaji wa taarifa ambazo hujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi .

Naye Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amesema marehemu Lukuvi alikuwa mbunge mkongwe aliyelitumikia Jimbo la Isimani kwa zaidi ya miaka 30, akieleza kuwa kifo chake ni pigo kubwa kwa Bunge, Serikali na Taifa kwa ujumla.

Viongozi mbalimbali pamoja na familia ya marehemu wamesema Lukuvi atakumbukwa kwa uzalendo, unyenyekevu na moyo wa kuunganisha watu, wakisisitiza kuwa urithi wake unapaswa kuenziwa kwa vitendo kwa kuendeleza misingi ya utumishi aliouishi.