Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imeanza kuweka mkazo mpya katika kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya makaa ya mawe, huku ikiwataka wadau wa sekta hiyo kuungana na kuanzisha chama maalumu kitakachorahisisha mawasiliano na uratibu wa masuala yao na Serikali.
Akizungumza leo Machi 30,2026 Jijini Dodoma kwenye kikao na wadau hao, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema lengo kuu la Serikali ni kuona rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi kwa kiwango kikubwa zaidi, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Nimewaita hapa tujadiliane njia rahisi ya kusaidia kuwapunguzia mzigo lakini pia na Serikali ipate mapato,” amesema Mavunde, akihamasisha mjadala wa wazi kuhusu maboresho ya sekta hiyo.
Ameeleza kuwa changamoto nyingi zinazowakabili wadau wa sekta ya makaa ya mawe zinaweza kupatiwa suluhisho kupitia umoja wao, akisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa chama hicho ndani ya muda mfupi.
“Suluhisho la changamoto hizi ni nyinyi kuanzisha umoja wenu,nategemea kuona hatua iliyofikiwa ndani ya wiki ijayo,” amesisitiza.

Waziri huyo ameongeza kuwa mapendekezo yatakayowasilishwa na wadau yanapaswa kulenga kuongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa, huku akiwataka kuwa tayari kuyasimamia kwa vitendo na hata kusaini makubaliano ya utekelezaji.
Aidha, amegusia uwepo wa masuala mtambuka yanayohusisha Wizara ya Fedha pamoja na sekta ya uchukuzi, akieleza kuwa ushirikiano wa karibu ni muhimu ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa sekta hiyo.
Kuhusu malalamiko ya mrabaha, Mavunde ameiagiza Tume ya Madini kushughulikia suala hilo kwa haraka na kuwasilisha majibu kwa wakati ili kutoa ufafanuzi unaohitajika kwa wadau.

Katika hatua nyingine, ametangaza kuwa kuanzia sasa hakutakuwa na bei elekezi ya makaa ya mawe itakayowekwa bila kushirikisha wadau, akionya kuwa kufanya hivyo kunaweza kudhoofisha biashara na kupunguza ufanisi wa soko.
Amebainisha kuwa Serikali imemteua mtu maalumu wa kushughulikia masuala ya makaa ya mawe, akiwataka wadau kuwasilisha hoja zao kupitia utaratibu huo ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka na wenye tija.




