Mkutano wa 13 wa Pamoja wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Ushirikiano katika Ulinzi, Amani na Usalama na Baraza la Kisekta la Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje umezikutanisha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujadili masuala muhimu ya kikanda leo Machi 30, 2026 jijini Nairobi, Kenya.

Brig. Jen. Anna Kerengi ameuongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Ngazi ya Wataalam uliowaleta pamoja Wataalamu wa Mabaraza Matatu ya Wizara zinazoratibu masuala ya amani, ulinzi, usalama na sera za mambo ya nje za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wataalamu hao wamejadili masuala mbalimbali mtambuka katika maeneo ya ulinzi, amani na usalama wa kikanda pamoja na uratibu wa Sera za Mambo ya Nje.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Mkutano, Dkt. Andrew Musiime kutoka Uganda amezitaka Nchi Wanachama kupitia Wizara husika kuyatekeleza kwa haraka maamuzi yote yatakayofikiwa ili kuleta maendeleo kwa wakati.

“Maamuzi mengi ya EAC huchukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa kutekelezwa, nahimiza Nchi Wanachama kuchukua hatua za makusudi na kwa wakati,” amesema Dkt. Msime.

Mkutano wa Ngazi ya Wataalam umeutangulia Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika Aprili Mosi na kisha Mkutano wa Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika Aprili 2, 2026.

Mkutano huu utapitia pamoja na mambo mengine Rasimu ya Mkakati wa Ushirikishwaji wa Wanawake katika masuala ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; kupokea taarifa kuhusu uandaaji wa Mfumo Jumuishi wa kielektroniki wa Tahadhari za Mapema wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; Mapendekezo ya Mpango wa ushirikishwaji wa Asasi za Kiraia, sekta binafsi na Taasisi za dini katika utekelezaji wa utaratibu wa jumuiya wa kuzuia, kusimamia na kutatua migogoro.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inategemea kuwakilishwa katika Mkutano wa ngazi ya Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.