Na Stella Aron JamhuriMedia, Ifakara
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imewaondolewa kero ya umeme ya kukatikatika mara kwa mara wakazi wa mji wa Ifaraka na Ulanga baada ya Kituo cha cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza umeme cha Ifaraka kukamilika kilichogharimu sh bilioni 25.
Hayo yamebainika leo Machi 31, 2026 wakati wa ziara ya wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA.
Wakili Daunstan Kyobya ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero,amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kumeongeza chachu katika kuchochea maendeleo kutokana na wananchi kuendelea na uzalishaji bila ya kusimama simama kama awali.

“Kabla ya ujenzi wa kituo tulikuwa tukitumia laini moja ya umeme kutoka Kidatu megawati 3.5 ambapo kulikuwa na changamoto kubwa kutokana na usafirishaji, lakini kwa sasa kero hiyo imeisha baada ya kuzalisha megawati 18 na kati ya hizo ni megawati saba pekee hutumika na zingine 11 hubaki.
“Hivyo sasa ni wakati wa wawekezaji kuja Ifakara kuwekeza kwani sasa tuna umeme usiokatikakati, na kuna fursa nyingi kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika.
“Kuna fursa za uwekezaji katika nyanja nyigi kama kwenye uchimbaji madini, utalii katika Hifadhi ya Nyerere, Udzungwa na fursa zingine ni kilimo cha ufuta, viungo, pamba, korosho, miwa na parachichi,” amesema.
Awali, Meneja wa Usimamizi wa Miradi REA, Mhandisi Deogratius Nagu amesema ujenzi wa kituo hicho umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Kilombero na Ulanga kwa kufungua zaidi shughuli za kiuchumi.
“Tunaishukuru serikali kupita REA kwa kutoa kiasi hicho cha fedha cha bilioni 25 ambazo zimetumika katika ujenzi wa kituo hicho ambacho kimemaliza kero ya umeme kukatikatika mara kwa mara na kuchangia maendeleo kuongezeka” amesema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile amesema uwekezaji unaofanywa na REA unaliondoa Taifa katika unyonge uliokuwepo miaka ya nyuma.
“Zamani ulikuwa ukisafiri ukiona mwanga ulikuwa unajua umefika mjini, lakini hali hiyo sasa ipo kila sehemu. Huu ni uwekezaji mkubwa uliofanyika,” amesema.
WANUFAIKA
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kilimo ya Wasichana ya Ifakara, Setina Ngailo amesema kuwa shule hiyo ni miongoni mwa taasisi zilizonufaika na ujenzi wa kituo hicho ambapo hivi sasa wanafunzi wanasoma nyakati za usiku na bila ya vikwazo.
“Wanafunzi hawajawahi kulala gizani, na wanapata muda zaidi wa kujifunza, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho tunaweza kusema kuwa kumechangia kuongeza ufaulu na pia umechangia uhakika upatikanaji wa maji muda wote hapa shuleni” amesema.

Naye msimamizi wa kiwanda cha kukoboa mpunga cha Buzelengule, Enos Machimu amesema uwepo wa umeme wa uhakika umechangia kuongeza idadi ya wateja kutokana na kupatikana kwa huduma bila ya vikwazo ukilinganisha na awali.
“Wakati umeme ulikuwa unakatika na kurudi tulikuwa tunakoboa tani tatu kwa siku, lakini sasa tunakoboa tani 22 na tunafanyakazi muda wote jambo ambalo limetusaidia kujikwamua kiuchumi”
Kwa upande wa Hospitali ya Rufaa ya Good Samaritan, msimamizi wa hospitali hiyo, Father Charles Massawe amesema kituo hicho kimesaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kwani awali walilazimika kutumia jenereta ambalo lilikuwa likitumia dizeli ya Sh500,000 kwa mwezi lakini hivi sasa imebaki ni historia.



