Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.Mwigulu Lameck Nchemba, amewasilisha Bungeni mpango wa mapato na matumizi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akiomba zaidi ya shilingi trilioni 12.5 kwa ajili ya kuendesha shughuli za Serikali.

Katika mgawanyo wa fedha hizo, kiasi cha trilioni 8.7 kimeelekezwa kwenye matumizi ya kawaida huku trilioni 3.7 zikitarajiwa kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu inalenga kukusanya mapato ya ndani yanayozidi trilioni 2.4 ndani ya kipindi hicho.

Akizungumza Bungeni leo Aprili 1,2026 Dodoma,ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuweka nguvu katika vipaumbele vinavyochochea ukuaji wa uchumi na ajira, hasa kupitia ushiriki wa sekta binafsi.

“Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, katika mwaka wa fedha 2025/2026 jumla ya miradi 927 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 11.08 ilisajiliwa, ishara ya kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji nchini, ” amesema

Amesema Katika sekta ya viwanda, ujenzi wa kongani ya Sino Tan Industrial Park umefikia asilimia 80, huku baadhi ya viwanda tayari vikianza uzalishaji. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya laki moja kwa Watanzania.

Serikali pia imeendelea kusisitiza mapambano dhidi ya rushwa, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 60 zimeokolewa kutokana na kudhibiti ubadhirifu na vitendo vya rushwa.

Vilevile, Waziri Mkuu amesisitiza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akiwataka wadau wote kuoanisha mipango yao ili kufanikisha malengo ya muda mrefu ya maendeleo.