Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Wakati wananchi wakitarajia utulivu wa gharama za maisha mwanzoni mwa robo ya pili ya mwaka, hali imekuwa tofauti baada ya kutangazwa kwa ongezeko kubwa la bei za mafuta nchini, hatua inayotishia kuongeza mzigo wa maisha na gharama za uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotoewa leo Aprili 1,2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)Dkt. James A. MMwainyekule,mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Aprili 2026 yamechochewa na mwenendo wa soko la kimataifa, ambapo bei za rejea (FOB) zimepanda kwa viwango vikubwa.

Takwimu zinaonesha kuwa petroli imeongezeka kwa asilimia 69.98, dizeli kwa asilimia 114.46, huku mafuta ya taa yakipanda kwa asilimia 120.81 ikiifanya dizeli kuwa bidhaa iliyoathirika zaidi katika ongezeko hilo.

Athari za ongezeko hilo tayari zimeanza kujitokeza katika soko la ndani ambapo Jijini la Dodoa na Dar es Salaam, bei ya petroli imefikia shilingi 3,820 kwa lita, dizeli 3,806, na mafuta ya taa 3,684 kwa lita.

Hali ni ngumu zaidi katika maeneo ya pembezoni mwa nchi, hususan mikoa ya Kagera na Kigoma, ambako bei za baadhi ya bidhaa zimevuka shilingi 4,000 kwa lita, zikichochewa na gharama za usafirishaji.

Ongezeko hili linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mvutano wa kisiasa na kijeshi katika ukanda wa Mashariki ya Kati Mgogoro unaohusisha mataifa ya Marekani, Israel na Iran ukitajwa kuathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji na usambazaji wa mafuta duniani.

Kufungwa kwa Mlango wa Hormuz njia muhimu inayosafirisha takriban asilimia 20 ya mafuta duniani kumezidisha uhaba wa bidhaa hiyo katika soko la kimataifa.

Sambamba na hilo, mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta, ikiwemo visima, maghala na mitambo ya kusafisha, yamesababisha kupungua kwa uzalishaji.

Aidha, gharama za usafirishaji zimeongezeka kufuatia uhaba wa meli za kubeba mafuta pamoja na kupanda kwa viwango vya bima kwa vyombo vya usafiri vinavyopita katika maeneo yenye hatari kubwa ya kiusalama.

Kupanda kwa bei za mafuta kunatarajiwa kuwa na athari pana kwa uchumi wa taifa, hususan katika sekta za usafirishaji, viwanda na huduma.

Ongezeko la gharama za nishati mara nyingi husababisha kupanda kwa bei za bidhaa na huduma nyingine, hali inayoweza kuongeza mfumuko wa bei na kupunguza uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha.

Katika kukabiliana na hali hiyo, wananchi wameaswa kutumia nishati kwa uangalifu zaidi, huku serikali ikiendelea kutafuta mbinu za kupunguza athari za mabadiliko hayo kwa jamii na uchumi kwa ujumla.

Pamoja na changamoto hizo, EWURA imeeleza kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta kukidhi mahitaji ya sasa, huku ikisisitiza ufuatiliaji wa karibu wa mwenendo wa soko la kimataifa ili kulinda maslahi ya watumiaji wa ndani.