Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange amezindua zoezi la upandaji wa miti kuelekea kumbukizi ya miaka 104 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere Aprili 11, 2026. Zoezi hilo limefanyika katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Aprili 01, 2026.
Akizungumza na viongozi, watumishi na wadau wa mazingira, Dkt. Dugange amesema kuwa katika kumuenzi Baba wa Taifa jamii haina budi kutunza mazingira kwani alikuwa ni mwanamazingira wa kweli.
Sanjari na hilo aliwahiza wananchi kupanda miti ili kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa mazingira.
Dkt. Dugange alisema kuwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za utunzaji wa mazingira ni muhimu kupanda miti na kuitunza ili kukabiliana na athari za mabadliko ya tabianchi zinazosababisha hali ya ukame na jangwa nchini.
“Nawahimiza wananchi tubadilishe utamaduni wetu tuanze sasa kupanda miti kila tunaposherehekea siku ya kuzaliwa kwani suala la kupanda miti ni muhimu na tukifanya hivyo tutapambana na kuenea kwa jangwa,” alisema.
Aidha, Naibu Waziri huyo aliipongeza Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kuratibu zoezi la upandaji miti.
Alisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha mazingira yanakuwa endelevu na kukabiliana na maradhi, hewa mbaya inayotokana na uchafuzi wa mazingira.
Aliongeza kuwa Serikali inatekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayozungumzia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhimiza matumizi matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuacha kutumia kuni na mkaa katika taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Bw. Peter Mavunde alisema katika zoezi hilo miti 200 kupandwa na miti 300 kupanda wakati wa kilele.
Alisema Aprili 13, 2026 litafanyika Kongamano la Vijana ambalo linalenga kuwajengea vijana uzalendo na kuwafanya wawe sehemu ya nchi na kuenga kizazi cha sasa na kijacho.
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Baraka Luvanda alisema zoezi la upandaji wa miti ni maono ya Hayati Mwalimu Nyerere katika hifadhi ya mazingira.
Balozi Luvanda alisema kuwa hatua hiyo inaunga mkono mpango kabambe wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa kukijanisha Tanzania na Mpango Kabambe wa Mazingira (2022-32).
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Bw. Dennis Simba alisema zoezi hilo ni uwekezaji wa kulinda mazingira kwani limesaidia upatikanaji wa mvua katika maeneo mbalimbali nchi.
Aliongeza kuwa Taasisi hiyo inaunga mkono Serikali katika kupunguza matumizi ya karatasi katika utendaji kazi kwa kuwa na mfumo wa manunuzi ya umma ya kijani kwa kutumioa mfumo wa NeST.





