KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdalla Hamid amewasilisha salamu za pole za Chama kwa Algeria, kutokana na kifo cha Rais Mstaafu wa nchi hiyo, Liamine Zeroual.
Rabia aliwasilisha rambirambi hizo leo Aprili 1, 2026 katika makazi ya Balozi wa Algeria nchini, Gharib Zermane na kutia saini kitabu cha maombolezo.
Serikali ya Algeria imetangaza siku tatu za maombolezo kutokana na kifo cha kiongozi huyo ambaye anatambuliwa kuwa mmoja wa viongozi walioacha alama muhimu Algeria hususan mfumo wa kidemokrasia.
Rais Mstaafu Zeroual alikuwa mmoja wa majemedari waliopigana vita vya kusaka uhuru wa Algeria kisha alichaguliwa kuwa rais wa mpito wan chi hiyo mwaka 1994.
Novemba mwaka 1995 Rais Zeroual aliandaa uchaguzi wa kidemokrasia ulioshirikisha vyama vingi vya siasa ambapo alikaa madarakani kwa miaka minne hadi Aprili 27, 1999 alipong’atuka.









