Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kupitia Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya hiyo (EASTECO), kwa kushirikiana na Baraza la Vyuo Vikuu la Afrika Mashariki (IUCEA) na wadau wa maendeleo, imetoa motisha ya kifedha kwa vijana wabunifu kama njia mojawapo ya kutambua mchango wao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kupitia teknolojia na kuwaongezea hamasa ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Wabunifu hao kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamejipatia kiasi cha dola za Marekani 10,000 kwa washindi wakuu, huku wengine wakipata dola 1,400 kila mmoja. Tuzo hizo zilitolewa katika Kongamano la Nne la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (4th EAC Regional Science, Technology and Innovation Conference) lililoandaliwa na EASTECO na kufanyika jijini Kigali, nchini Rwanda.
Akizungumza katika hafla ya kufunga kongamano hilo, Waziri wa Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Ubunifu wa Rwanda Mhe. Paula Ingabire alieleza kuwa kazi za ubunifu za vijana hao, zilizowezeshwa na teknolojia, zimechangia kutatua changamoto katika sekta mbalimbali, zikiwemo elimu, kilimo, utunzaji wa mazingira, afya na usafirishaji. Aidha, aliendelea kutoa wito kwa Nchi Wanachama kuendelea kuwaunga mkono vijana na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za ubunifu, hususan kupitia matumizi ya Akili Unde (AI).
Vilevile, katika kuendelea kuhamasisha matumizi ya AI ndani ya Jumuiya, kongamano hilo lilipitisha maazimio 15 yenye lengo la kuhakikisha fursa zitokanazo na AI zinatumika ipasavyo, ili kuimarisha mtangamano na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha uchumi.
Miongoni mwa maazimio hayo ni pamoja na kuboresha sera, mifumo na mikakati ya kitaifa ya AI; kuimarisha ujuzi wa AI katika Jumuiya; kuanzisha na kuimarisha Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Teknolojia Zinazoibukia; kuanzisha Mfuko wa Kikanda wa Teknolojia ya AI kwa ajili ya utafiti; kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi katika teknolojia ya AI; kuendeleza miundombinu ya pamoja ya kikanda ya AI; na kuanzisha mifumo ya usimamizi wa data pamoja na miundombinu ya pamoja.
Maazimio mengine ni pamoja na kuanzisha Jukwaa la Kikanda la Viongozi wa Kidijitali litakalowakutanisha wadau mbalimbali ili kuratibu juhudi za kitaifa na vipaumbele vya kikanda vya AI na masuala ya kidijitali; kukuza vipaji vya ubunifu; na kuhimiza maadili katika ubunifu na matumizi ya AI.






